Habari ni taarifa halisi juu ya matukio mbali mbali yanayojiri ulimwenguni ambayo mtu anahaitaji kusikia, kuona au kusoma kwa lengo la kupata taarifa Fulani.
Haki ya kutafuta, kutoa na kupokea habari ni haki ya msingi ya mwanadamu iliyoainishwa kwenye Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 kifungu cha 18 (1) na (2) ambavyo vimeeleza kuwa kila mtu ana haki ya kupewa taarifa wakati wowote kuhusu matukio mbali mbali nchini na duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi, na pia juu ya masuala muhimu kwa jamii.
Picha kutoka Maktba
Vyombo hivyo ni pamoja na Umoja wa Mataifa
(UN), Muungano wan chi za Amerika (OAS), Baraza la Ulaya (CE) na Umoja wa
Afrika (AU).
Licha ya sheria, sera pamoja na mikataba
mbali mbali juu ya uhuru na haki ya kutafuta taarifa na kuzisambaza kwa umma,
lakini bado kuna sheria ambazo ni kandamizi kwa vyombo vya habari na wanahabari
kwa ujumla.
Miongoni mwa Sheria hizo ni sheria nambari
5 ya 1988 ya Usajili wa Mawakala wa Habari, Magazeti na vitabu iliyofanyiwa
marekebisho na sheria nambari 8 ya 1997, kifungu cha Sheria cha 27 (1) kifungu
hichi kinampa mamlaka afisa yeyote wa Polisi kuweza kukamata gazeti lolote,
popote litakapoonekana, lilipochapwa au kuchapishwa au ambalo kwa maoni yake
atalituhumu kwamba limechapwa au kuchapishwa, kinyume na sheria hii.
Kifungu hichi kinaonesha wazi jinsi ambavyo vyombo
vya habari na uhuru wa wanahabari unavyoingiliwa na kukandamizwa kwakumpa
mamlaka kupitiliza afisa yeyote wa Polisi ambaye kwa bahati mbaya anaweza kuwa
hana taaluma ya habari wala utambuzi wa sheria zilizompa uhuru mwandishi wa
habari katika kutekeleza majukumu yake au kulipiza kisasi.
WADAU WA HABARI WANASEMAJE JUU YA KIFUNGU HIKI.
Kwa upande wake mwandishi wa habari
mwandamizi Zanzibar Rashid Omar Kombo, amesema kifungu cha sheria kinachomruhusu
afisa wa Polisi kuchunguza mchakato wowote au utendaji wa masuala ya habari kinyume
na hati ya mahakama ni Sheria zinazokinzanza na mikataba mbali mbali ya kikanda
na kimataifa juu ya uhuru wa vyombo vya habari.
“Kimsingi
mataifa yote ya kidekrasia ambayo yanafuata misingi ya demokrasia na utawala
bora masuala ya afisa wa polisi kukamata na kukagua yanahitaji idhini na vibali
vya mahakama afisa wa Polisi hawezi kuwa yeye ndiye anatuhumu na yeye ndiye
anakamata hiyo itakuwa ni Sheria ya ajabu” amesema
Fathiya Mussa Said ni mratibu wa chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania Kisiwani Pemba (TAMWA), amesema uwepo wa kifungu cha sheria kinachompa mamlaka afisa yoyote wa Polisi kufanya ukaguzi wa majengo pamoja na kukamata gazeti ni kifungu cha sheria ambacho inakandamiza uhuru wa vyombo vya habari na wanahabari kwa ujumla.
Fathiya Mussa Said Mratibu wa Tamwa Pemba.
“Kiufupi naweza kusema kwamba ni sheria ambayo inapaswa kufanyia marekebisho kwani imeshapitwa na wakati kulingana na uhataji uliyopo sasa hivi kutokana na aina ya vyombo tulivyonavyo” amesema
MAONI YA WAHARIRI WA VYOMBO VYA HABARI.
Bakari Mussa Juma ni mkuu wa gazeti
la Zanzibar leo Kisiwani Pemba, ametoa ushauri kwa waandishi wa habari
kuendelea kupaza sauti ili kufanyiwa marekebisho kwa sheria ambazo zinaonaka
kukinzana na uhuru wa vyoombo vya habari na wanahabari.
“Hajalisha kwamba tumepiga kelele sana juu ya sheria hizi lakini
tusichokee niwasihi waandishi wenzangu tuendelee kupaza sauti mpaka tuhakikishe
kuwa zimefanyiwa marekebisho” Bakar Mussa
Mhariri wa Hits fm Radio Moza Saleh Ali, ameeleza kuwa kutokana na
mabadiliko ya sayansi na teknolojia sheria kama hizo ni sheria kandamizi kwa tasnia
ya habari, hivyo basi ameviomba vyombo vya sheria kuzifanyia marekebisho sheria
hizo.
“Kwa mujibu wa wakati tuliona nao sheria kama hizi zionanekana ni sheria kandamizi kwa vyombo vya kwasababu nyakati zimebadilika kwa wakati ule pengine inafaa ila kwa wakatii sheria hiyo haiyendani na mazingira” alieleza
KLABU ZA WAANDISHI WA HABARI ZINA
MAONI GAZI JUU YA KIFUNGU HIKI.
Ali Mbarouk Omar ni Mwenyekiti wa
Klabu ya waandishi wa habari Pemba (PPC), amesema mkataba wa Afrika wa haki za
binadamu na watu ya mwaka 1981 ibara ya 9 na 19 zinatoa haki ya mtu kutafuta na
kupokea taarifa pasi na uhuru wake kuingiliwa, hivyo kuendelea kuwepo kwa wa
sheria hiyo kuna kwenda kinyume na makubaliano ya mkataba huo, hivyo basi
ameshauri sheria hiyo kufanyiwa marekebisho haraka iwezekanavyo.
Nae Katibu wa jumuiya ya waandishi wa
habari za maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA) Salma Said, amesema kuendelea kutumika
kwa sheria zisizozingatia uhuru wa vyombo vya habari ni miongoni mwa sababu
zinazopelekea waandishi wa habari kufanyiwa matendo mbali mbali ya unyanyasaji
ikiwemo kutekwa, kupigwa na hata kuawa.
“Ukiacha na hicho kifungu cha 27 kuna sheria nyingi sana ambazo hazikuzingatia
uhuru wa vyombo vya habari wala usalama wa waandishi wa habari na ndio maana
waandishi wa habari leo wanatekwa kiholela, wanapikwa na wengine kuuawa” Salma
Said
MAONI YA BARAZA LA HABARI TANZANIA-ZANZIBAR.
Shifaa Said Hassan ni afisa mdhamini Baraza la Habari Tanzania-Zanzibar (MCT) amesema katika utaratibu wa kisheria afisa wa Polisi anapaswa kupewa kibali na mahakama kukagua jengo au kukamata gazeti, hivyo basi Sheria ambayo inampa mamlaka afisa yeyote wa Polisi kukagua jengo na kukamata gazeti kwa kwa maoni yake ni sheria inayokwenda kinyume uhuru wa vyombo vya habari na wanahabari kwa ujumla.
“Katiba ya Zanzibar ya 1984 ibara ya 18 imeruhusu kila mwananchi kuwa huru katika kutafuta na kusambaza habari ndani na nje ya nchi wakati wowote bila ya kuingiliwa na mtu yeyote, sasa Sheria ya namna hiyo ni Sheria inayo kwenda kinyume na hata katiba yetu” alifafanua
MAONI YA WAANDISHI WA VYOMBO MBALI MBALI VYA HABARI.
Waandishi wa habari kutoka vyombo mbali mbali vya habari wamesema kuendelea kuwepo kwa Sheria zisizo rafiki kwa vyombo vya habari kutapelekea waandishi kufanyakazi kwa khofu, jambo ambalo litapelekea taarifa wanazoandika kukosa usahihi
“Kama afisa yeyote wa Polisi amepewa mamlaka ya kukagua na kukamata hadi daftari la kumbukumbu la mwandishi kuangalia ameandika kitu gani ni lazima waandishi tutakuwa na khofu na hatutofanya kazi kwa ufanisi” alisema mmoja wa waandishi hao
MAONI YA WAUZAJI WA MAGAZETI KISIWANI PEMBA.
Baadhi ya wauza magazeti maarufu
kisiwani Pemba, wamesema sheria inayomtaka mchapishaji wa magazeti yanayochapwa
Zanzibar kuwasilisha nakala mbili kwa kwa mrajis kwa gharama zake kila siku
anapochajisha gazeti ni Sheria inayorudisha nyuma biashara ya uuzaji wa
magazeti pamoja kampuni za uchapaji.
“Aina hiyo ya Sheria inarudisha nyuma kwa kiasi kikubwa biashara ya
uchapishaji wa magazeti pamoja na uuzaji, kwasababu na mchapishaji wa magazeti
anatumia gharama na muda kuposti nakala hizo kila siku” muuza magazeti maarufu eneo la Chake
Chake
MAONI YA WASOMAJI WA MAGAZETI.
Idawaonline.com ilizungumza na baadhi
ya wasomaji wa magazeti kisiwani Pemba, juu ya sheria hiyo na kusema endapo
Sheria hizo hazitofanyiwa marekebisho zitapelekea wananchi wengi kukosa habari
kwa wakati, hivyo basi wamependekeza Sheria hizo kufanyia mabadiliko
‘’Kiasi kikubwa sana wananchi tunategemea vyombo mbali mbali vya habari
kwa ajili ya kupata taarifa mbali mbali zinazojiri ndani na nje ya nchi punde
tu zinapojiri sasa kama kuna Sheria kama hizo ambazo zinaonekana kuminya uhuru
wa vyombo vya habari na wanahabari kufanya kazi zao wananchi tutashindwa kupata
habari kwa wakati” alisema
mmoja wa wasomaji hao
NINI KIFANYIKE ILI KUREKEBISHA SHERIA HIZO.
Wadau wa habari nchini wamekuwa wakichukua
hatua kadhaa ikiwemo kuandaa makongamano mbali mbali kushinikiza kufanyiwa
marekebisho kwa sheria hizo hususan katika kuadhimisha siku ya uhuru wa habari
duniani.
Miongoni mwa wadau hao ni pamoja na Chama cha Waandishi wa habari Wanawake Tanzania (TAMWA-Zanzibar) na shirika la habari la Internews Tanzania kwakuazisha mradi wa miezi sita (6) kwakushirikiana na Waandishi wa habari Visiwani Zanzibar katika kuongeza uchechemuzi ili kufanyiwa marekebisho kwa sheria ambazo zinazonekana sio rafiki kwa vyombpo vya habari na wanahabari kwa ujumla.
Mwisho.