Makamu Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Zanzibar Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema hatua ya Chama chake kuingia katika Serikali ya Umoja wa kitaifa (GNU), haikuwa kwa dhamira ya kujipatia nafasi za uongozi, bali ni kwa kujali maslahi ya Taifa.
Mheshimiwa Othman ambayepia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ameyasema hayo leo akizungumza na Wafuasi wa Chama hicho, katika Hafla ya Ufunguzi wa Jengo Jipya la ACT-Wazalendo, Jimbo la Tunguu, Mkoa wa Kati kichama, kisiwani Unguja.
Amesema kuwa maslahi hayo ni pamoja maridhiano ya kisiasa, umoja na utetezi wa kweli juu ya haki na maslahi makubwa ya Zanzibar, sambamba na kuijengea Tanzania mazingira bora ya kuleta mageuzi.
Ameeleza kuwa mambo mengi yanayoendelea kujiri sasa katika mnasaba wa mageuzi Nchini, siyo bure bali ni juhudi za makusudi za Chama pamoja na dhamira njema ya kuyafanikisha.
Aidha amewahimiza wanachama na wafuasi wa ACT-Wazalendo kuendeleza umakini katika utekelezaji wa dhamira ya muda mrefu ambayo ni pamoja na kupigania mamlaka kamili ya Zanzibar akisema, "uwekezaji mnaoufanya ni muhimu sana na unatosha kuyafikia matarajio muda ukifika".
Akiongea juu ya dhana ya mabadiliko yenye tija kwa maslahi ya Taifa, Mheshimiwa Othman amesema, "hakuna mzalendo wa kweli anayehofia mageuzi bali ukiona mtu anahofia mageuzi huyo hana uchungu wowote na nchi".
"Nasema Chama chetu ni chama cha mageuzi na hakiwezi kuyumba, tumejipanga kupigania mageuzi hayo", amesisitiza Mheshimiwa Othman huku akitaja hatua za hivi karibuni Chama hicho kilipokutana na Vikosi-kazi mbali mbali vya kuratibu maoni ya kuleta mabadiliko, ambavyo ni pamoja na Umoja wa Ulaya (EU).
Naye Naibu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo Zanzibar ambaye pia ni Waziri wa Afya Zanzibar Mheshimiwa Nassor Ahmed Mazrui, ametoa wito kwa wafuasi wa Chama hicho kuepuka nongwa, na kusema wasione shida kujumuika katika hafla za Serikali katika kuhamasisha maendeleo.
Ameongeza kuwa ACT-Wazalendo ni Chama chenye umakini wa kupambanua baina ya harakati za Serikali na Chama, na kwamba isiwe shida kujipambanua kiitikadi pale inapobidi, kwa kuzingatia Maslahi na Nia ya kutetea Mamlaka kamili ya Zanzibar.
Kwa upande wake, Mdhamini wa Ujenzi wa Jengo hilo, Mwanasheria Mkuu wa ACT-Wazalendo ambaye pia ni Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Mheshimiwa Omar Said Shaaban ameeleza kuwa miongoni mwa azma za kutekeleza hatua hiyo ni pamoja na kwamba Chama hicho ni mbadala wa kuiongoza Tanzania Bara na Visiwani.
Sherehe hizo zimewahusisha Viongozi mbalimballi wa Chama hicho ambao ni pamoja na Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano ya Umma, Bw. Salim Bimani
Imetolewa na,
Kitengo cha Habari,
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.
Julai 23,2022.