Wananchi Kisiwani Pemba wametakiwa kutumia njia mbadala ya amani na haki katika utatuzi wa migogoro wa kesi za madai ili kuendelea kudumisha amani na haki nchini.
Mapema akizungumza na wananchi wa Kijiji
cha Kibubunza Shehia ya Shumba Muhogoni Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini
Pemba, Afisa programu kutoka taasisi ya Foundation For Civil Society “FCS” Evelyn
Mchau, alisema taasisi ya Foundation For
Civil Society kwa kushirikiana na kituo cha huduma za sheria Zanzibar “ZLSC”
zimedhamiria kuwajengea uwezo wananchi juu ya namna bora ya utatuzi wa migogoro
kwa njia shirikishi na majadiliano ili kuendelea kudumisha amani na haki
nchini.
Aidha alisema suala la migogoro ni
suala linalomgusa kila mmoja katika jamii, hivyo basi amewaomba wananchi hao
kuwa na utaratibu nzuri wa usuluhishi katika utatuzi wa migogoro inayowakabili.
“Ukichunguza vyanzo vingi vya migogoro mingi katika jamii zetu inatokana wanajamii kutofautiana kisha kushindwa kukaa pamoja wakasuluhisha na badala yake kukimbilia kwenye vyombo vya sheria, niwaombe sana musifanye hivyo pindi munapotofautiana na badala yake kutaneni na musuluhishane wenyewe” Evelyn Mchau
Kwa upande wake, Mratibu wa Kituo cha huduma za sheria Zanzibar upande wa Pemba Safia Saleh Sultan, alisema njia nzuri ya wananchi kuepukana na migogoro na na uvunjifu wa amani ni kukaa pamoja na kusuluhishana wenyewe ili kuepukana na chuki pamoja na visasi.
Ameongeza kuwa, miongoni mwa sababu zinazopelekea
kutoweka kwa amani nchini ni uwepo wa migogoro mbali mbali katika jamii ikiwemo
migogoro ya ardhi, mashamba pamoja na familia.
Alisema “Naomba niwasihi sana ndugu
wananchi munapokuwa na migogoro mbali mbali kama vile migogoro ya ardhi, mashamba
pamoja na familia kaeni pamoja musuluhishane badala ya kuanza kuchukiana na
kuchukuliana sheria mikononi hiyo ni mbaya sana”
Nae, wakili kutoka kituo cha huduma
za sheria Zanzibar tawi la Pemba Siti Habib Mohammed, aliwasihi wananchi hao
kuzifanyia suluhu wenyewe kesi za madai kwani kuzipeleka katika vyombo vya
sheria husababisha ugomvi na uhasama.
Aidha wakili huyo, alisema amewaasa
wana kijiji hao kutokuzifanyia suluhu kesi za jinai ikiwemo kesi za
udhalilishaji.
“Kwahivyo niwaombe pindi munapokuwa
na kesi za madai ni vyema mukasuhisha wenyewe badala ya kupelekana kwenye
vyombo sheria ispokuwa kwa kesi za jinai hususan kesi za udhalilishaji” alishauri
Ali Abdalla Ameir ni mwananchi wa
kijiji hicho, ameomba elimu ya usuluhishi wa migogoro kwa njia ya amani
kutolewa mara kwa mara ili wananchi wawe na uwezo nzuri wa kutatua migogoro
inayojitokeza kwa njia ya haki na utulivu
“Ni washukuru sana kwa ujio wenu
kwetu kwakweli tumejifunza mambo mengi sana kuhusiana na sheria na njia bora ya
utatuzi wa migogoro kwa njia amani, niwaombe leo isiwe mwisho muwe munakuja
mara kwa mara ili wananchi wazidi kupata elimu hii na waweze kuitumia”
alishauri
Mwanakijiji Ali Abdalla Ameir akiulizwa maswali Kwa Maafisa wa ZLSC na FCS.
Afisa ufuatiliaji na tathmini kutoka “ZLSC” Zanzibar Khamis
Haroun Hamad, amewataka wananchi kushirikiana katika utatuzi wa kesi za madai
zinazotokezea katika maeneo yao.
Nao baadhi ya wananchi walisema
wanakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo changamoto mipaka ya mashamba
pamoja na rushwa kwa upande wa kesi za madai.
Akifunga mkutano huo, sheha wa shehia
hiyo Salim Said Salim, amawashukuru maafisa kutoka ‘ZLSC’ na ‘FCS’ kwa
kuwafikia wananchi hao katika kuwapatia elimu hiyo adhimu ya utatuzi wa
migogoro kwa njia ya usuluhishi.
“Kwa niaba ya wananchi wa kijiji cha
Kibubunza, niwapongeze watendaji wa Kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar ‘ZLSC’ kwa
kuja kwenu kutoa elimu hii kwa wananchi” alieleza
Akieleza namna ya utatuzi wa migogoro
kwa njia ya usuluhishi, mratibu wa ‘ZLSC’ Pemba Safia Saleh Sultan, alisema
miongoni mwa njia bora za wananchi kutatua migogoro inayowakabili ni pamoja na
kuwatumia wazee, viongozi wa dini, vikao vya familia, watu maarufu pamoja
wasaidizi wa huduma za sheria.
Kituo cha huduma za Sheria Zanzibar ‘ZLSC’ kwa kushirikiana
shirika la Search For Common Ground ‘FSC’ wanaendesha mradi wa mwezi mmoja wa
utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala za amani na haki,, unaofadhiliwa na na
taasisi ya Foundation For Civil Society ‘FSC’.
Mwisho.