Watu wenye ulemavu kisiwani Pemba wametakiwa kushiriki kikamilifu katika zoezi la kuhesabu watu na makaazi ‘Sensa’ linalotajiwa kuanza Agosti 23 ili nao waweze kujumuishwa katika mipango ya maendeleo.
Mapema akizungumza na viongozi wa
jumuiya mbali mbali za watu wenye ulemavu huko katika ukumbi wa idara ya
mazingira Machomanne kisiwani Pemba, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Kwanza
wa Rais Zanzibar Mhe. Harusi Said Suleiman, amesema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti
wa baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesisitiza na kuwapa kipaumbele
watu wenye ulemavu nchini ili waweze kujumuishwa katika mipango ya maendeleo ya
Serikali.
Aidha, amewaomba wazazi na walezi kutokuwaficha
watoto wenye ulemavu pamoja na kuficha aina ya ulemavu walionao ili waweze kupatiwa
haki yao ya msingi ya kuhesabiwa.
“Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi kasisitiza sana na katupa kipaumbele cha
kutosha kwamba jamai muhakikishe munawafikia watu wenye ulemavu kwani ni watu
muhimu katika mipango ya maendeleo na akasema sote ni walemavu watarajiwa”
alisema
Sambamba na hayo, amewaomba viongozi
hao kupambana na vitendo vya udhalilishaji kwa watu wenye ulemavu ili
kuhakikisha wanaepukana na janga la udhalilishaji ambalo linaonekana kukithiri
visiwani Zanzibar.
“Lakini niwaombe tuwe tayari
kupambana na hili janga la udhalilishaji ambalo limeingia katika nchi yetu, wanadhalilshwa
watu wenye nguvu zao, wenye macho yao, wenye viungo vyao, wenye akili zao seuze
sisi ambao tuna mapungufu fulani, kwahivyo niwaombe ndugu zangu tulisimamie kwa
pamoja” alisema
Kwa upande wake, mwenyekiti wa watu wasio ona Zanzibar kisiwani Pemba Suleiman Mansour, amesema watu wenye ulemavu kisiwani Pemba wamelipokea vyema zoezi Sensa na kuomba makarani wa Sensa kuwa kauli nzuri kwa watu wenye ulemavu ili kufanikisha zoezi hilo ipaswavyo.
Pia, amemuomba Mheshimiwa waziri kufikisha
salamu na ombi kwa Mheshimiwa rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa baraza la
Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi kuwaangalia kwa jicho la huruma watu wenye
ulemavu ikiwemo kuwajengea ofisi zenye kuendana na mahitaji yao.
Yahya Mohammed Seif ni mtu mwenye ulemavu wa uziwi, ameiomba Ofisi ya mtakwimu mkuu wa kutoa takwimu za watu wenye ulemavu ili waweze kutambua idadi ya watu wenye ulemavu nchini na aina ya ulemavu walionao.
Nae, katibu wa jumuiya ya wasioona Wilaya ya Chake Chake Said Abdalla Sadi, ameahidi huwashajihisha watu wenye ulemavu kushiriki kikamilifu katika zoezi la Sensa pamoja kupambana hali na mali dhidi ya vitendo vya udhalilishaji kwa watu wenye uelamavu.
Mratibu wa Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu Kisiwani Pemba Mashavu Juma Mabrouk, akiwasihi washiriki wa Mkutano huo kutoa mashirikiano Kwa makarani wa sensa.
Zoezi la Sensa ya watu, makaazi linatarajiwa kuanza Agosti 23 kuanzia saa za usiku.
Sense kwa maendeleo, jiandae kuhesabiwa.
Mwisho.
-