Wahitimu 16 wa darasa la lugha na utalii wameombwa kiutumia vyema fursa ya lugha za kigeni walizojifunza katika soko la utalii ili mafunzo hayo yaweze kuwaletea maendeleo.
Akihutubia katika mahafali hayo huko katika skuli ya sekondari ya
Uweleni Mkuu wa Wilaya ya Mkoani Mheshimiwa Khatib Juma Mjaja, amesema lugha
ndio fursa pekee ambayo inatoa fursa nyingi za ajira katika soko la ajira,
hivyo basi amesema kuanzishwa kwa kituo hivyo vya lugha za kigeni kutasaidia
kwa kiasi kikubwa kukuza soko la utalii nchini.
“Ni waombe sana kuitumia fursa hii
lugha katika kujiajiri katika sekta ya utalii ambayo ina fursa za kutosha kwa
vijana ambao wana uwezo nzuri wa kuzungumza lugha zaidi ya moja lakini
kujiajiri kwenu kutaleta ushawishi kwa vijana wengine kupata moyo wa kujiunga
na darasa hili” DC Mjaja
Kwa upande wake, mwenyekiti wa mahafali hayo, Abdalla Saleh Issa, amesema lengo la kuanzishwa darasa
hilo ni kuwawezesha vijana katika umahiri wa kuweza kutumia lugha mbali mbali
za kigeni ili kuendana na soko la utalii ndani na nje ya Zanzibar.
Ameongeza kuwa, wazo la kuanzishwa
kwa darasa hilo la lugha limetokana na Mkuu wa Wilaya ya Mkaoni Mheshimiwa
Khatib Juma Mjaja wakati alipokuwa afisa mdhamini wizara ya Utalii na Mambo ya
Kale kisiwani Pemba, ambapo wazo hilo limefanikiwa kuwasaidia vijana zaidi ya 50 kutoka wilaya ya Mkoani.
“Lakini ndugu wahitimu munaemuona
hapa licha ya kuwa mgeni rasmi alikuwa ndio afisa mdhamini wizara ya utalii na
mambo ya kale, kwahivyo madarasa haya yaliasisiwa chini yake ilikuwa ni rai
yake yaanzishwe madarasa haya” Alisema
Nao, wahitimu wameahidi kufanyia kazi
ipaswavyo mafunzo ikiwemo kujiendeleza kimasomo sambamba na kujiajiri katika
sekta ya utalii.
Lugha zinazofundishwa katika darasa
hilo ni pamoja na lugha ya Kiarabu, Kiingereza, Kifaransa pamoja na Kitaliano.
Hayo ni mahafali ya tatu (3) tangu
kuanzishwa kwa kituo hicho cha lugha za kigeni na utalii Mtambile.
Jumla ya wanafunzi 16 wamehitimu darasa la lugha za kigeni na utalii na kutunukiwa vyeti vitakavyo wawezesha kujiendeleza na masomo ya lugha mbali mbali pamoja na kuomba ajira katika soko la utalii.
Mwisho.