Walimu wa madrasa wameombwa kufundisha somo la maadili katika madrasa zao na katika jamii ili kupunguza idadi ya matukio ya vitendo vya udhalilishaji nchini.
Mapeama akifungua mafunzo ya siku
moja kwa walimu wa madrasa huko katika Skuli ya Sekondari ya Idriss Abdul Wakil Kizimbani Wete Pemba yaliyoandaliwa na jumuiya ya maendeleo ya walimu wa madrasa Pemba 'JUMWAMPE', Mkuu wa Wilaya ya Wete Mhe.
Hamad Omar Bakar, amesema kukithiri kwa vitendo vya udhalilishaji kunachangia kwa
kiasi kikubwa kuporomoka kwa maadili sambamba na upotevu wa nguvu kazi kwa taifa.
Ameongeza kuwa Wilaya ya Wete ni
miongoni mwa Wilaya inayoongoza kwa idadi ya matukio ya vitendo vya udhalilishaji
kisiwani Pemba huku ikiwa inashika nafasi ya pili visiwani Zanzibar.
“Kwahivyo ndugu waalimu nahisi sasa
kuna ulazima wa kuanzisha utoaji wa elimu ya maadili ili wanafunzi pamoja na
jamii iweze kuifahamu elimu pamoja na kuwa na khofu ya Mungu ili tuweze
kupunguza matukio ya udhalilishaji” alishauri
Mkuu wa Wilaya ya Wete Hamad Omar Bakari akizungumza na waalimu wa madrasa walioshiriki katika Mafunzo hayo.
Kwa upande wake, Mkuu wa divisheni ya
utawala, mipango na rasilimali watu Said Khalfani Issa, alisema walimu wa
madrasa ni watu mihimu katika malezi ya jamii, hivyo basi wanapaswa
kujitambua ili waweze kuepukana na vitendo viovu ikiwemo vitendo vya
udhalilishaji.
“Nyinyi ndio muhimili wa jamii katika mambo mbali mbali ikiwemo kusimamia na tabia za watu katika jamii zetu kwahivyo muna umuhimu mkubwa mno, lakini ili umuhimu huo uonekane munapaswa kujitambua nyinyi ni nani na muna nafasi gani katika jamii” Said Khalfan Issa
Akiwasilisha mada juu ya umuhimu wa
kuweka kumbukumbu za fedha katika madrasa Khator Ali Abdalla, amewasisitiza
waalimu hao kuwa na uwezo mzuri wa kujua hesabati pamoja kuweka kumbukumbu
katika uwekaji na matumizi ya fedha ili kuepukana na migogoro inayojitokeza
mara kwa mara.
Alisema “Tumekuwa tukisikia kesi
nyingi sana kuhusu matumizi mabaya ya utumiaji wa fedha katika madrasa, hivyo
basi kupitia wasilisho hili nadhani mumejifunza umuhimu na namna bora uwekakaji
wa kumbukumbu za fedha ili kuondoka na kesi zinazojitokeza mara kwa mara”
Nae, Mkurugenzi wa jumuiya ya
Mazingira na Utetezi wa Kijinsia Pemba ‘PEGAO’ Hafidh Abdi Said wakati akiwasilisha
mada juu ya Uongozi, alisema ili kiongozi aweze kuwa kiongozi bora anapaswa
kuwa na sifa ya kuona mbali, kushirikiana na anaowaongoza, kuwa na moyo wa
kujitolea pamoja na kukubali kukosolewa.
“Kiujumla kuna sifa nyingi sana zinazomfanya
kiongozi kuwa bora kama mulivyozitaja lakini, hizo sifa nne ambazo nimezitaja
hapo juu ndio sifa kuu ambazo kiongozi anapaswa kuwa nazo ili nafasi yake ya
uongozi aweze kuitumikia iapaswavyowa, kwahivyo nawaomba sana waalimu
muzizingatie sifa hizo” Hafidh Abdi Said
Aidha aliwasihi waalimu hao kuachana
na tabia ya kujibagua na kujiona bora kutokana na kutofautiana na misingi ya
kimadhehebu ili kuepukana na migogoro pamoja na mipasuko inayojitokeza mara kwa
mara.
Akiwasilisha mada juu ya njia bora za
utatuzi wa migogoro Salum Hamad Shaib, aliwaomba waalimu hao kukaa meza moja
pindi wanapotofautiana na wazazi na walezi ili kuweza kuitatua migogoro
inayojitokeza kwa njia ya amani na haki.
Alishauri “Kama tunavyojua kuwa suala
la migogoro ni suala ambalo haliwezi kuepukika katika maisha ya mwanadamu,
lakini inapotokezea tofauti niwaombe mukae meza moja ili muweze kumaliza
tofauti zenu kwa njia ya amani na haki”
Akitoa nasaha kwa waalimu hao
mwenyekiti wa jumuiya ya maendeleo ya waalimu wa madrasa Pemba Hamad Ali Hamad,
amewasihi waalimu hao kuachana na tabia ya kulumbana, kuchukiana sambamba na
kuwafanyia husda wanafunzi wao wenye ufahamu nzuri wa masomo ili waweze kupata
wasaidizi wazuri katika majukumu yao.
Nao, waalimu hao wameahidi kuyafanyia
kazi ipaswavyo mafunzo ili yaweze kuwanufaisha wao na jamii kwa ujumla.
Mafunzo hayo ya siku moja yameadaliwa na jumuiya ya maendeleo ya waalimu wa madrasa Pemba ‘JUMAMPWE’ yameshirikisha waalimu wa madrasa 87 kutoka shehia 32 za Wilaya ya Wete Pemba.
Baadhi ya walimu wanawake walioshiriki katika Mafunzo hayo.
Mwisho.