Na Hamida Kamchalla, TANGA.
CHAMA cha Wananchi (CUF) kimetaka katiba mpya inayolinda kipengele cha kufanyika mikutano ya hadhara kama ilivyo kwenye katiba iliyo po na kupiga marufuku jeshi la polisi kuingilia na kuzuia mikutano hiyo isifanyike.
Wito huo ameutoa Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Sheria, Salvatory Magafu katika mkutano wa viongozi wa Wilaya zote za Mkoa wa Tanga wa chama hicho na kusema serikali imekanyaga katiba kwani kuruhusu jeshi la polisi kuzuia mikutano ya hadhara ni kitu ambacho hakipo katika katiba ya Jamuhuri ya Muungano.
Magafu amesisitiza kuwa jukumu la jeshi hilo libaki kulinda usalama wa raia na mali zao bila kuingilia mikutano hiyo kama wanavyofanya kwenye shuhuli za harusi au zingine za kijamii.
"Mikutano ya hadhara ipo kwa mujibi wa katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, ibara ya 20, kwahiyo tunaomba iheshimiwe, ibara hii inampa mamlaka hata raia wa kawaida kuitisha mkutano wa hadhara, mikutano ya vyama vya siasa isimamiwe na vyama pekee, sheria na muongozo wa uendeshaji wa jeshi la polisi visihusike kusimamia mikutano hiyo" amesema.
"Hivyo basi, vifungu vya sheria namba 11 na 12 ya vyama vya siasa vifutwe, jukumu la jeshi la polisi lisiwe kutoa au kutotoa kibali kwakuwa kibali cha mikutano hiyo kimeshatolewa na katiba iliyipo, na bila shaka hii tunataka iendelee kuwepo kwenye katiba mpya" amesisitiza Magafu.
Aidha Magafu amefafanua kwamba kutokana na katiba kuvunjwa mara kadhaa na chama kilichopo madarakani wananchi wengi wameshachoshwa na uongozi wa mabavu hivyo basi kwa sasa wamesimama imara na hawawezi tena kuvumilia hali hiyo na kwamba wanasubiri kuona Rais wa awamu ya sita ana maamuzi gani juu ya tamko la katiba mpya.
"Kutoka mwaka 2015 hadi 2021 nchi hii ilikuwa haiongozwi kisheria bali iliongozwa kwa utashi wa mtu, alisema mwanzo, mwisho, sasa wao wanafikiri kwamba kile kipindi ndicho kitakachoendelea, tutafika mahali uvumilivu utatushinda kwa kipindi hiki" amesema.
"Tunashukuru kwa kipindi hiki Rais wetu Samia Sulluhu Hassan ni msikivu na anatusikiliza, sasa tunasubiri tuone na yeye maamuzi yake kuhusu katiba mpya yatakuwa ni yapi, tulishaitisha mabaraza na kutoa matamko yetu mojawapo ni kutoshiriki uchaguzi mkuu nchini, mpaka pale tutakapopata Tume huru ya uchaguzi na katiba mpya, huo ndio msimamo wetu na hatujauondoa" amebainisha.
Naye Katibu Mkuu (CUF), Hamad Masoud Hamad alisema msimamo wa kutoshiriki chaguzi kuu nchini utakwisha endapo mikutano ya hadhara itapatiwa ufunbuzi lakini wakati mchakato ukiendelea, chama kinajipanga madhubuti kwa ajili ya uchaguzi kuanzia mwaka 2024 na kuhakikisha ushindi unapatikana katika nafasi mbalimbali.
Amefafanua kwamba Amani katika nchi ndiyo nguzo imara kwani nchi bila Amani hakuna kitu chochote kinachoweza kufanyika katika kuliletea Taifa maendeleo hivyo wanasubiri kupata majibu ya utaratibu ambao Rais anashuhulika nao.
"Na tunashukuru Rais Samia ametuwekea utaratibu kiasi ambacho kwenye tundu ya sindano unaona meanga upande wa pili, kwahiyo tuna Imani, tumpe muda na muda ambao siyo mrefu suala hili la mikutano ya hadhara litakuwa mjadala umefungwa" amesema.
Hamad pia amesema, "suala hilo ndilo hasa ambalo linafanya chama kunadi sera zake kwa wananchi na kwa anayependezwa na sera zake, kinapata wanachama".
Lakini pia alisisitiza na kuwataka wananchi wote kujitokeza siku ya sensa, "tukumbuke tunaelekea kwenye sensa, hii haina itikadi ya chama, kwahiyo Watanzania wote hili suala letu sote, tarehe 23 mwezi huu, tujitokeze kuhesabiwa na tuhesabiwe kwasababu sensa ni mpango wa Kitaifa ili kupata taarifa za kutosha na takwimu sahihi ili nchi iweze kupanga mipango ya maendeleo ya Taifa letu" amesema.
Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Pangani akiongea na viongozi wenzake katika mkutano huo.
Viongozi wa Wilaya wa Chama cha Wananchi CUF, Mkoa wa Tanga wakifuatilia mkutano.