KIZAZI CHEMA HUANDALIWA KAMA MBEGU IPANDWAVYO SHAMBANI – MHE. OTHMAN

Hassan Msellem
0

MAkamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Alhaj Othman Masoud Othman, amekumbusha wajibu wa wazazi juu ya umuhimu wa malezi mema ya watoto, ili kujenga ustawi bora wa jamii, na kwaajili ya kuwekeza katika kizazi chema cha baadaye. Alhaj Othman ameyasema hayo leo alipowasalimia waumini wa Dini ya Kiislamu huko Masjid Taqwa, Msikiti uliopo Amani Magogoni, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, mara baada ya Ibada ya Swala ya Ijumaa.


Amewakumbusha Waislamu na Wananchi kwa ujumla, kufahamu kwamba wema katika jamii hautopatikana kwa matarajio ya kuchipuka ukubwani, bali utapatikana kwa kupanda mbegu njema kupitia malezi mema mithili ya mazao ambayo yanaoteshwa shambani kwa kutaraji mavuno bora.


Amesema kwamba jamii kamwe isitarajie kupata viongozi wema na waadilifu pasipo kuwaandaa watoto ipasavyo kupitia malezi bora, na kwamba hatua hiyo ndiyo inayoisadia kupanda mbegu njema kupitia makuzi yao.


Mheshimiwa Othman amefahamisha kwamba kupitia viongozi wema ndani ya jamii ndipo hupatikana wafuasi wema, na hivyo waumini hawanabudi kutafakari kwa kutilia maanani suala la malezi bora kupitia jitihada za makusudi, sambamba na kuwakuza vyema vijana kimaadili, tangu hatua za awali za maisha yao.


“Ndivyo ilivyo kwamba mbegu bora hupelekea matunda bora, kama ilivyo kwa malezi mema ya watoto, hatimaye hupatikana viongozi wema ambapo na wafuasi wao pia watakuwa ni wema, na hapo tutapata jamii na nchi ya watu wema”, amefahamisha Mheshimiwa Alhaj Othman.


Mapema akitoa Khutuba Mbili za Swala ya Ijumaa, kwa waumini waliohudhuria katika Ibada hiyo, Khatiib wa Msikiti huo, Sheikh Nassor Mohammed Juma, amewahimiza waislamu kuyahama maovu yote, na kujilazimisha kuishi katika maisha mema kupitia vitendo vyema vinavyokubalika katika jamii na katika Dini ya Kiislamu. Kiongozi huyo amesema jukumu la msingi la mzazi ni katika kuchunga na kusimamia tabia za vijana ambao ni sehemu kubwa ya familia, na wala haipaswi kuwanyooshea vidole viongozi pekee kwa kuwatupia lawama, kutokana na ukweli kwamba suala la kuporomoka kwa maadili linagusa wajibu wa kila mtu ndani ya jamii.Kitengo cha Habari.

Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,

Agost 05, 2022.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

 


 

 
#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top