Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam linamshikilia kijana Gadi Daudi maarufu kwa jina la 'Tito' au 'Jeshi la mtu mmoja' (28) Mkazi wa Ubungo Riverside kwa tuhuma za kumuua Manafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Julius Fredrick (22) na kumpora simu yake ya mkononi.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Jumanne Muliro amesema tukio hilo lilitokea Julai 16, 2022 majira ya saa kumi usiku katika eneo la karibu na hosteli za Magufuli Wilaya ya Ubungo Dar es Salaam baada ya kumvizia, kumshambulia na kitu chenye ncha kali sehemu mbalimbali za mwili, kupora vitu vyake ikiwemo simu na kumsababishia kifo.
Kamanda Muliro amesema baada ya kumuhoji kwa kina Mtuhumiwa alikiri kumuua mwanafunzi huyo na kumpora vitu vyake na alikiri pia kufanya matukio kama hayo ya unyanganyi kwenye maeneo tofauti ya jiji la Dar es Salaam
Hata hivyo, Uchunguzi wa Jeshi la Polisi umebaini kuwa mtuhumiwa huyo ni mhalifu sugu ambaye amekuwa akifanya matukio ya kiuhalifu maeneo ya Mlimani city, Mwenge na Kawe, na aliwahi kushtakiwa kwa kesi ya Unyang'anyi wa Kutumia Silaha Kesi namba 256/2020 na kufungwa miaka 30 kuanzia Julai 6, 2020, na aliachiwa huru Aprili 2022 kwa sababu za kisheria baada ya kukata rufaa.