Hivyo basi amesema wameona kuna haja ya kutoa mafunzo hayo kwa waandishi wa habari ili waweze kuifikisha elimu hiyo kwa wananchi.
‘’Tumegundua kuwa wananchi wengi hawana elimu juu ya maradhi yasiyoambukiza na ndio maana vifo vimekuwa vingi kwahivyo tumeona kuna haja ya kutoa mafunzo haya kwenu ili muweze kuyafikisha katika jamii kwasababu nyinyi munaifikia jamii moja kwa moja’’ alisema
Aidha amesema, Miongoni mwa maradhi yasiyoambukiza na yanayosababisha vifo kwa wingi ni pamoja na Kisukari, shinikizo la damu, pamoja na Saratani ya matiti kwa akina mama.
‘’Kila mwaka wanawake zaidi ya 300,000 wanakufa kutokana na saratani ya shingo ya kizazi kwa utafiti uliofdanywa na shirika la afya duniani’’ alisema
Kwa upande wake, afisa kutoka kitengo cha maradhi yasiyoambukiza Zanzibar Rabia Ali Makame, amesema Miongoni mwa sababu zinazopelekea kuongezeka kwa wimbi la maradhi hayo ni pamoja na ulaji usiofaa, kutokufanya mazoezi pamoja na utumiaji wa tumbaku na vileo.
‘’Asilimia 60% ya magonjwa yote ya saratani yanahusishwa na mtindo wa maisha na mazingira ikiwemo ulaji usiofaa, matumizi ya tumbaku, matumizi ya Pombe, mionzi hatari pamoja na kutokufanya mazoezi’’ Rabia Makame Ali
akichangia mada katika mafunzo hayo, mwandishi kutoka gazeti la Zanzibar leo Abdi Suleiman, amesema hali duni ya maisha pamoja kukosa uelewa juu ya ujali bora ni miongoni mwa sababu zinazopelekea kuongezeka kwa maradhi yasiyoambukiza.
‘’Kwa mfano unaikuta familia ina watoto kumi au zaidi baba hana kazi rasmi ya kujipatia kipato ni kwa namna gani anaweza kuwa na uhakika wa ulaji bora wa familia yake’’ alihoji
Alisema‘’Wananchi wengi hawana elimu sahihi ya mapishi na ujali bora unamkuta mtu anapika mboga ya mchicha au matembele lakini anaiosha mpaka inachujuka kisha anaipika na kuimwaga maji hivi kwa upishi huo lishe itapatikana kwali’’
Akitaja vichocheo vya maradhi yasiyoambukiza, amesema ni pamoja na umri, jinsia na historia familia ambapo maradhi hayo hurithiwa kutoka kizazi kimoja hadi chengine.
‘’Kwahivyo maradhi haya yasiyoambukiza yana mnasaba mkubwa na vitu hivyo vitatu ambavyo ni umri yani watu wenye umri kuanzia miaka 50 na kuendelea wako hatarini zaidi kupata maradhi haya lakini pia jinsia kwa mfano maradhi ya saratani ya matiti kwa kawaida wanapata sana wanawake kuliko wanaume na tenzi dume hivyo hivyo na historia ya familia pia endapo katika familia au ukoo kuna mtu aliwahi kuugua maradhi fulani kuna uwezekano mkubwa na wewe kupata maradhi ya aina hiyo’’ alifafanu
Takwimu zinaonesha watu milioni 12 kila mwaka hugundulika na Saratani ulimwenguni kote.
Maradhi ya Saratani inaongoza kwa vifo duniani kote, inakadiriwa vifo zaidi ya milioni 10 vimetokea katika mwaka 2020 ambapo ni sawa kati ya watu 6 mmoja hufariki kwa saratani.
Akitaja sababu zinazosababisha maradhi ya shinikizo la damu, amesema husababishwa na engezeko la nguvu ya msukumo wa damu katika mishipa inayochukua damu kutoka kwenye moyo kwenda sehemu nyengine za mwili.
Utafiti uliofanywa na wizara ya afya Zanzibar umeonanesha kuwa watu wenye umri kati ya miaka 25 hadi 65, sawa na asilimia 33 wanaishi na shinikizo la damu na asilimia 3.7 wanaishi na ugonjwa wa kisukari.
kwa mujibu wa takwimu za shirika la afya duniani ‘WHO’ mwaka 2021, zinaonesha kuwa maradhi yasiyoambukiza yanauwa watu milioni 41 kila mwaka ambayo ni sawa na asilimia 71 ya vifo vyote duniani kote na mwaka 2020, jumla ya vifo 684, 996 vilitokana na saratani ya matiti.
Ili kupunguza uwezekano wa saratani ya shingo ya kizazi ni pamoja na kuepuka kushiriki tendo la ndoa kinyume na kufika umri wa miaka 18, kuepuka uvutaji wa sigara na tumbaku kupunguza uzito wa ziada pamoja na kuacha matumizi ya mafuta kwa wingi.
Nao, waandishi hao wameahidi kufanyia kazi mafunzo hayo sambamba na kuyafikisha kwa jamii ili waweze kujikinga na maradhi yasiyoambukiza.
Mafunzo hayo ya siku mbili yaliyotolewa na kitengo cha maradhi yasiyoambukiza Zanzibar yaliyojumisha waandishi wa habari 23 kutoka vyombo mbali mbali vya habari
Mwisho.