Mvua inayoendelea kunyesha mkoani Geita inayoambatana na upepo, radi imepelekea vifo vya watu watatu wa familia moja na mmoja kujeruhiwa na radi katika kitongoji Cha Idoselo kijiji cha Kasesa kata ya Kaseme Jimbo la Busanda Wilaya ya Geita Mkoani Geita Agosti 16, 2022
Akizungumzia tukio hilo mtoto wa familia, Naomi James amesema mvua ilianza kunyesha majira ya saa tano asubuhi ambapo mama yake mzazi Melesiana Ludeba (56) pamoja na Bibi yake Magema Koma (78) na mjukuu wao Kelvin Shadrack mwenye Umri wa mwaka mmoja walikuwa ndani wamepumzika ndipo aliposikia kelele Moja halafu utulivu ukatawala
"Mama yangu (Malesiana Ludebe) alikuwa ndani ya chumba, ghafla radi ikapiga, ndio kwenda kuwaangalia nikakuta wamezimia, madaktari walipokuja wakawapima, wakatuambia weshafariki," amesema Naomi
Naye baba wa familia hiyo, James Lubiyu amesema "Kipindi mvua inanyesha nilikuwa nje ilikuwa mvua ya kawaida mke wangu ,mama mkwe pamoja mjukuu wangu walikuwa ndani sikuiona Nilishtukia tu wengine waliokuwa ndani wanapinga kelele ".
"Baada ya kuingia ndani nikaona wote wanne waliopata ajali hiyo wamezimia nikaita viongozi na daktari akafika pale wakaniambia wameshafariki watatu mke wangu (Maleciana Lubede (56) Mama mkwe Magema koma (78) pamoja na Mjukuu wangu mmoja tu alinusurika".
Kwa upande mwenyekiti wa kitongoji wa Idoselo, Jackson Mchele amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambalo limeshangaza watu wengi kwa kuwa ni miaka mingi hawajashuhudia tukio Kama hilo.
Mbunge wa Jimbo la Busanda Mhandisi Tumaini Magesa amefika kuwapa pole wafiwa wa familia hio katika Kitongoji Cha Idoselo na kuwaomba wawe na subira katika kipindi hiki kigumu.
Mhandisi Magesa aliwaomba kuchukua tahadhari hasa kwenye kipindi hiki cha mvua zinazoendelea kunyesha mkoani humo