Baada ya taarifa hii kuripotiwa na gazeti la mwananchi hatimae serikali imetolea ufafanuzi na kutaka mwanafunzi huyo kufika kesho muhimbili kuchukua kitambulisho chake. na hii ni sehemu ya Habari katika gazeti la Mwananchi.
Mwanafunzi wa Chuo cha Serikali za Mitaa (LGTI), Hombolo mkoani Dodoma, Lightness Shirima (22) amesema anahangaika kulipa deni la matibabu la Sh9 milioni aliloliacha baba yake aliyefariki dunia Hospitali ya Mloganzila ili apatiwe kitambulisho chake cha uraia (Nida).
Lightness (Pichani), ambaye anasoma chuoni hapo mwaka wa pili LGTI, alisema hivi karibuni kuwa baba yake, Priscus Shirima alifariki dunia Julai 4, mwaka huu katika hospitali hiyo jijini Dar es Salaam baada ya kulazwa kwa siku 40 na kuacha deni.
Ili kuwa na uhakika deni hilo litalipwa, uongozi wa hospitali hiyo unadaiwa kumtaka mwanafunzi huyo kutoa kitambulisho cha Nida kama dhamana na kupewa mwili wa baba yake kwa sharti la kulipa Sh50,000 kila mwezi.
Uongozi wa hospitali hiyo ulikiri kuidai familia hiyo Sh9 milioni gharama za matibabu mgonjwa kukaa chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU) kwa siku 40 mfululizo.
Hii hapa kauli ya serikali kutoka waziri Ummy Mwalimu kupitia ukurasa wake Wa Instagram aliyoitoa agosti 8 2022.
Serikali ya Rais @samia_suluhu_hassan inajali wananchi wake. Mwenye mawasiliano na huyu bint anipatie inbox. Kesho saa 4 asubuhi afike Hospitali ya Taifa Muhimbili -Mloganzila akachukue kitambulisho chake, Akamuone Mkurugenzi wa Hospitali ya Mloganzila
Wakati ni kweli kuwa Sera ya Afya ya mwaka 2007 inataka wananchi kuchangia huduma za Afya bado Serikali inatambua kuwa wapo wananchi wengi ambao hawawezi kumudu gharama za matibabu hususani katika kipindi hiki cha maendeleo ya sayansi na teknolojia ambapo matibabu yana gharama kubwa. Ili kutatua changamoto hii Serikali inakuja na Sheria ya Bima ya Afya kwa kila mtu (Universal Health Insurance) ili kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma za afya bila ya kikwazo cha fedha.
Ni matumaini yetu kuwa tukiwa na utaratibu huu wa Bima ya Afya kwa kila mtu (wananchi wengi wazima watachangiana kidogo kulipia wananchi wachache watakaokuwa wagonjwa tofauti na sasa ambapo zaidi ya asilimia 90 ya wananchi wanaojiunga na Bima kwa hiyari ni wagonjwa) masuala haya tutayapunguza kama sio kuyamaliza kabisa.
Pia narudia tena kuzitaka Hospitali zote za Serikali nchini kuzingatia maelekezo ya @wizara_afyatz kuwa kila baada ya siku chache kuprint bill ya mgonjwa (mteja) ili ndugu waweze kulipia na hii itasaidia kuwapunguzia mzigo wa kulipa bill kubwa za matibabu kwa mgonjwa wao. @gersonmsigwa