Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania Tamwa Zanzibar, kimesema licha ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi kuanzisha mahakama maalum ya makosa ya udhalilishaji bado vitendo vya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia vimekuwa vikiongezeka kwa kasi nchini.
Kauli hiyo imetolewa na mratibu wa
Tamwa Kisiwani Pemba Fathiya Mussa Said katika mkutano huo na wana mtandao wa
kupinga vitendo vya udhalilishaji Pemba, amesema utafiti wa kihabari uliofanywa Tamwa Zanzibar, mwaka 2020 umebaini kuwa vitendo vya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia bado ni tatizo
linaloikabili Zanzibar, ambapo jumla ya kesi 788 zimeripotiwa katika Wilaya zote
za Unguja na Pemba.
Ameongeza kuwa, miongoni mwa sababu
zinazopelekea kukithiri kwa vitendo vya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia ni
pamoja na matumizi mabaya mitandao ya kijamii, kukaa vijiweni pamoja na utumiaji
wa dawa za kulevya.
“Ripoti ya Tamwa Zanzibar ya mwaka 2020 imabainisha kuwa vitendo vya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia bado ni tatizo sugu, ambapo jumla ya kesi 788 Zanzibar zimeripotiwa kuanzia mwezi January hadi May, hii ikijumisha matukio ya ubakaji 692, kulawiti 100 na kunajisi 96 ambapo wahanga ni watoto walio chini ya umri wa miaka 18” alisema
Akiwasilisha ripoti ya kota ya pili
kuanzia mwezi January hadi May, katibu wa wana mtandao kutoka wilaya ya Mkoani Shaaban
Juma Kassim, amesema kuanzia mwezi January hadi May 2022, jumla ya kesi kumi
(10) zimeripotiwa ambapo miongoni mwa kesi hizo kesi tatu (3) zimeondolewa, kesi
mbili (2) ziko katika Polisi, kesi mbili (2) zimesuluhishwa kwenye familia,
moja (1) mtuhumiwa ametoka, moja (1) iko kwa mwendesha mashtaka na moja (1)
ikisalia mahakamani.
“Katika ripoti hii tumefanikiwa kurekodi matukio kumi ambayo yanatoka katika shehia mbali mbali kesi nyingi zilizoripotiwa ni kesi za ubakaji, shambulio la aibu pamoja na utelekezaji” alieleza
Siti Faki Ali mwana mtandao kutoka
Wilaya ya Wete, amesema katika pindi cha mwaka January hadi May 2022, jumla ya
kesi 29 ambapo kesi za kubaka kumi na nne (14) kutorosha sita (6) shambulio la
aibu nne (4) ujauzito moja (1) kumuingilia maharimu nne (4).
Aidha, amesema kutoka mwezi June hadi Agosti 2022, wamefanikiwa kuripoti kesi kumi na tatu (13) ambapo kesi za kubaka ni saba (7) kutosha moja (1) udhalilishaji wa kingono moja (1) kumpa mimba mwari nne (4).
Nae, afisa wa dawati la jinsia Wilaya
ya Mkoani, amesema miongoni mwa changamoto zilizojitokeza katika kupambana na
kesi za udhalilishaji ni pamoja wanajamii kuzisuluhisha kesi hiyo wenyewe na
endapo wakishindwa kukubaliana ndipo wanakwenda katika vyombo vya sheria, jambo
ambalo linapelekea watuhumiwa kutoroka.
Sambamba na hilo, amesema suala la kukataa kutoa ushahidi kwa waathirika wa vitendo vya udhalilishaji pamoja na mashahidi ni miongoni mwa changamoto zinazozikabili kesi hizo, kwani kukosekana kwa ushahidi kunapelekea kesi hizo kufutwa.
Ripoti hiyo ya robo mwaka ambayo pia
ilikuwa na muendelezo wa kesi mbali mbali zinazoendelea mahakamani na zile
zilizoripotiwa vituo vya Polisi, imetolewa na wana mtandao kutoka wilaya Wete
na Wilaya ya Mkoani Pemba, ambapo imeonesha kasi ya vitendo vya udhalilishaji
wa kingono na kijinsia kuendelea kushamiri.
Mradi huo wa miaka miwili (2) wa
kutumia jukwaa la habari kumaliza udhalilishaji Zanzibar, unatekelezwa na chama
cha waandishi wa habari Tanzania ‘Tamwa, Zanzibar, ambao unafadhiliwa na Shirika
la kimataifa la maendeleo la Denmark (DANIDA) kupitia ubalozi wa Denmark
Nchini.
Mwisho.