Mahakama ya wilaya ya Muheza mkoani Tanga,leo imewahukumu Tano Charles (30) pamoja na Mayunga Makelege (25) wakazi wa wilaya ya Nzega mkoani Tabora kutumikia kifungo cha miaka 30 jela kila mmoja kwa kukutwa na kosa la kusafirisha kilogramu 31 za madawa ya kulevya aina ya Bangi.
Mbali na kutoa hukumu hiyo pia Mahakama hiyo imeamuru kilogram hizo 31 za Bangi zichomwe Moto mapema iwezekanavyo kuanzia sasa.
Kosa hilo la kusafirisha madawa hayo ya kulevya aina ya Bangi linatajwa kufanyika mnano tarehe 22/02/2022 majira ya saa 9:30 jioni wakati watenda kosa hao walipokuwa kwenye gari la abiria namba ya T 734 AFD scania kampuni ya J ROYAL kutoka Morogoro ambapo walikamatiwa eneo la Mvuleni wilayani Muheza mkoani Tanga.
Hukumu hiyo imetolewa leo Agosti 18,2022 na Hakimu mkazi wa Mahakama ya wilaya ya Muheza, Yusuph Abdallah Zahoro kwa mujibu wa sheria ya kupambana na kuzuia madawa ya kulevya ,kifungu cha 15A(1)2C (sura ya 95 rejeo la 2019).
Hakitoa hukumu hiyo leo, hakimu mkazi mfawidhi wa wilaya ya Muheza alisema kwamba mahakama imewatia hatiani washtakiwa hao kwakuwa ushahidi umethibitisha bila kuacha shaka yoyote kuwa washtakiwa ndio watenda kosa hilo la kusafirisha kilogramu hizo za bangi kwa lengo la kuzifikisha sanjari na kuziuza mkoani Tanga.
Baada ya hukumu hiyo, akizungumza mwendesha mashtaka Michael Msangawale alisema kwamba madawa ya kulevya kwa ujumla yamekuwa na athari hasi katika jamii hivyo Hukumu hiyo ya leo Mahakamani hapo inaenda kutoa fundisho kubwa katika jamiii kwa wote wenye tabia kama hizo za kujihusisha na biashara hiyo kwa namna moja ama nyengine.