WANANCHI WAMETAKIWA KUANDAA TAARIFA ZAO KWA SAHIHI ILI KUHARAKISHA ZOEZI LA SENSA LINALOENDELEA NCHINI.
Wananchi Kisiwani Pemba wametakiwa
kuendelea kuweka kumbukumbu za watu waliolala katika kaya zao usiku wa kuamkia
Agosti 23 ili makarani wawafikiapo waweze kupata taarifa sahihi na za haraka
katika kaya zao.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa
habari huko katika ukumbi wa mkutano wa bodi ya mapato Zanzibar ‘ZRB’ Gombani
Pemba juu ya uendeleaji wa zoezi la sensa, Kamisaa wa sense Zanzibar balozi
Mohammed Haji Hamza, amesema zeozi hilo linaendelea vizuri kama lilivyopangwa licha
ya uwepo wa malalamiko ya baadhi ya wananchi waliotaraji kuhesabiwa siku ya
mwanzo ya zoezi hilo.
“Kama alivyoeleza Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dk. Hussein Ali Mwinyi juzi mara
baada ya kuhesabiwa kuwa sio watu wote watahesabiwa siku ya tarehe 23 Agosti, pekee
ndio maana zoezi hili limepangwa kufanyika kwa siku saba” alifafanua
Mhariri wa Gazeti la Zanzibar Leo Kisiwani Pemba, Ndg. Bakari Mussa Juma, akiwasilisha Dondoo katika mkutano huo.
Ameongeza kuwa, ikiwa leo Agosti 25 ni siku ya tatu ya zoezi hilo asilimia 35 ya kaya zote zimeshahesabiwa nchini.
“Kwa ufupi zoezi limeanza vyema na
linaendelea vizuri kama lilivyopangwa. Hadi leo asubuhi tarehe 25 Agosto, 2022
kupitia mfumo wa ufuatiliaji wa ukusanyaji wa taarifa za Sensa (The 2022
Population and Housing Census Monitoring Dashboard) kituo cha kuchakata taarifa
kilichopo Dodoma zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 35 ya kaya zilizopo nchini
zimeshahesabiwa” alisema
Aidha, amewaomba wananchi kuendelea
kuwa na subra juu ya zoezi hilo ambalo linatarajiwa kukamilika Agosti 29/2022
na endapo kutakuwa na mwananchi ambaye atakosa kuhesabiwa itatolewa nambari
maalumu ya simu ili mwananchi huyo aweze kutoa taarifa na kutimiza haki yake ya
kuhesabiwa.
Amewasisitiza kuwa kila kiongozi mmoja
wa shehia anapaswa kuongozana na karani mmoja ili kuharakisha utendaji wa zoezi
hilo.
“Uzoefu tuliupata tangu tarehe 23 Agosti, kuwa kuna baadhi ya viongozi hao wanalazimisha kuongoza makarani zaidi ya mmoja jambo ambalo linachelewesha zoezi hilo” alisema
Mwandishi wa Habari kutoka Kituo Cha Radio Istiqama FM Radio Salum Ali Msellem, akifuatilia Mkutano huo.
Sambamba na hayo, amevishukuru vyombo vya habari kwa kazi kubwa wanayoifanya ya utoaji wa habari pamoja na uhamasishaji wa wananchi juu ya zoezi la sensa ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Serikali juu ya umuhimu wa zoezi hilo.
“Naamini sana kuwa utoaji wa habari
kupitia vyombo vya habari pamoja na uhamasishaji ni kielelezo tosha cha jinsi
vyombo vya habari vinavyotambua na kuunga mkono juhudi za Serikali juu ya
umuhimu wa Sensa ya Watu na Maakazi” alieleza
Kwa upande wake, Mwenyekiti Bodi ya Takwimu Zanzibar Balozi Amina Sulum Ali, amesema muamko wa wananchi juu ya zoezi la sensa kwa mwaka 2022 umeongezeka ukilinganisha miaka iliyopita, hivyo basi amewaomba wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa makarani wa sensa ili lengo la zoezi hilo liweze kufikiwa.
Zoezi la kuhesabu watu na makaazi ‘Sensa’
hufanyika kila baada ya miaka kumi (10) kitaifa, ambapo lengo la Serikali
katika zoezi hilo ni kuweza kufahamu idadi ya watu na makaazi katika mipango ya
maendeleo endelevu ya taifa.
Zoezi hilo limeanza Agosti 23, 2022 na
linatarajiwa kukamilika Agosti 29, 2022.
Mwisho.