ALIYEHUKUMIWA MIAKA 5 JELA KWA KULOGA MTOTO WA MDOGO WAKE AACHIWA HURU

0

Mahakama kuu Kanda ya Iringa Imetengua hukumu ya kifungo cha miaka mitano (5) jela  kilichokuwa kinamkabili John Severine Chale (60) mkazi wa kijiji cha Iwela wilayani Ludewa Mkoani Njombe kwa kosa la kumloga na kumsababishia Ukichaa mtoto wa mdogo wake.


Kesi hiyo namba 11 ya mwaka 2022 ambayo ilitolewa hukumu Agosti 29 mwaka huu katika mahakama ya wilaya ya Ludewa mbele ya hakimu Isaac Ayengo na mwendesha mashtaka Asifiwe Asajile baada ya mtuhumiwa kukutwa na hatia. 


Akisoma hukumu hiyo kwa njia ya mtandao Jaji Mfawidhi wa Mahakama kuu Kanda ya Iringa Dkt. John Utamwa huku mshtakiwa aliyehukumiwa akifuatilia shauri hilo akiwa katika mahakama ya wilaya ya Ludewa amesema mahakama kuu ililazimika kuita hukumu ya shauri hilo kwaajili ya rejea na kujiridhisha endapo mwenendo wa shauri pamoja na hukumu vilizingatia sheria.


Amesema baada ya kurejea vifungu vya sheria mahakama hiyo imejiridhisha kuwa kifungu cha sheria namba 3 ya mwaka 2022 kilichotumika katika kutoa hukumu hiyo hakipo hivyo mahakama inakubaliana na maelezo ya wakili wa serikali Basilius Namkambe aliyeitaka mahakama hiyo kubatilisha hukumu hiyo.


Ameongeza kuwa John alishitakiwa chini ya kifungu namba 5 ambapo kifungu hicho kilikosewa kwakuwa sheria hiyo inazungumzia uchawi lakini maelezo ya kesi hiyo yalimtaja mshtakiwa kujihusisha na vitendo vya kishirikina na kushindwa kutofautisha ushirikina na uchawi.

 

Jaji Dkt. Utamwa amesema kutokana na makosa hayo mahakama imebatilisha mwenendo wa shauri hilo na kutengua adhabu ya kifungo hicho aliyopewa John Severine Chale kwakuwa adhabu hiyo imekwenda kinyume na matakwa ya sheria namba 5(1)(a) kinachoelekeza adhabu ya kifungo kisichopungua miaka 7 kwa makosa ya kichawi ambayo mshtakiwa huyo alishitakiwa nayo.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

 

 
#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top