Mama mmoja aliyefahamika Kwa jina la Faida Fadhili Ali anayekadiriwa kuwa na umri wa Miaka 70, mkaazi wa Kilimahodi Shehia ya Matale Wilaya Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba, amefariki dunia akiwa juu ya mkarafuu ikidhaniwa kuwa alitaka kuanguka na kukwama katika kamba aliyokuwa akiitimia kuchumia karafuu na kuchomwa na kisha jiti la ubavu lililopelekea kutokwa na damu na kupoteza Maisha.
Tukio Hilo limetokea September 15, 2022 majira ya saa 4 za Asubuhi katika bonde Kidongo Mkadini Shehia ya Matale.
Nassor Salum Mohammed ni shuhuda wa tukio hilo ambaye pia alishiriki kumkwamua Mama huyo kwenye mkarafuu huo, amesema alipata taarifa ya mama huyo kutaka kuanguka mkarafuu na Kisha kukwama ndipo alipokwenda na kumkuta akiwa amekwama na kamba aliyokuwa akiitimia kuchumia karafuu na Kisha kuchomwa na jiti la ubavu lililopelekea kutokwa na damu nyingi na kufanikiwa kumshusha akiwa tayari ameshapoteza maisha.
"Ilikuwa ya saa 4:30 za asubuhi nilipigiwa simu kuwa katika bonde la Kidongo Mkadini Kuna mtu ameanguka mkarafuu lakini amekwama ndipo nikakimbilia haraka kufika naangalia juu naona kweli Kuna mama amekwama na ananing'inia ndipo nikapanda juu haraka na kushirikia na wenzangu watatu kumshusha, alitaka kuanguka Kisha kukwama na kamba aliyokuwa anaitimia kuchumia na Kisha kufanya kama kupinda Kwa nyuma na kuchomwa na jiti la ubavu na kutokwa na damu nyingi labda ndilo lililopelekea kupoteza Maisha" alisema
Akikiri kutokea kwa kutio hilo Sheha wa Shehia ya Matale Mwalim Haji Mchande, amesema Majira ya saa 4:30 wakati akiwa kwenye kikao alipata taarifa za kutokea kwa tukio hilo la kuanguka kwa mama huyo na kufika katika eneo la ajali na kumkuta marehemu akiwa amelazwa chini na kufinikwa kanga.
Aidha Sheha huyo, ametoa wito kwa wananchi ambao wazazi wao wameshakuwa na umri mkubwa kutokuwaruhusu kufanya kazi ngumu ikiwemo uchumaji wa karafuu Ili kuepukana na ajali zisizo za lazima.
Nae, mtoto wa marehemu huyo anaefahamika Kwa jina la Juma Khatib Juma, amesema ameguswa sana na tukio hilo la kuondokewa na Mama yake mzazi kwani licha ya kuwa alikuwa Mzee lakini alikuwa akimsaidia mambo mbali mbali ikiwemo ushauri pamoja na nasaha katika maisha yake.
Mwili wa marehemu huyo, umehidhiwa kando kidogo na yaliyokuwa makaazi yake katika Kijiji cha Kilimahodi Jana September 15, 2022 Majira ya saa 10 za jioni.
Matukio ya watu kupoteza maisha yamekuwa yakijitokeza mara kadhaa kila ugikapo msimu wa uchumaji wa zao la karafuu Kisiwani Pemba, ambapo mwaka 2021 watu watatu walifariki Kwa kuanguka mikarafuu.