Waandishi wa habari Kisiwani Pemba wameombwa kuelimisha jamii juu ya athari zinazotokana na kuwanyanyapaa wahisiwa wa maradhi ya kuambukiza ya Kifua Kikuu, Uviko19 na wanaoishi na Virusa vya Ukimwi ili kuepukana na madhara yatokanayo na kuwanyanyapaa wahisiwa wa maradhi hayo.
Mapema Akizungumza na Waandishi wa Habari huko katika Ukumbi
wa Maabara ya Afya ya Jamii Wawi, Kaimu Mratibu wa Kifua Kikuu na Ukimwi
Zanzibar, Valeria Rashid Haroub, amesema miongoni mwa sababu zinazosababisha
kuongezeka kwa maradhi ya kuambukiza ni tabia ya kuwanyanyapaa wahisiwa wa
maradhi hayo hali inayopelekea kuwa na visasi vya kuyaambukiza maradhi hayo kwa
wengine.
“Takwimu zinaonesha kuwa waathirika wengi wa maradhi ya
kuambukiza ikiwemo HIV inatokana na tabia ya kuwanyanyapaa watu walioambukizwa maradhi
hayo, jambo ambalo linamfanya aliyeambukizwa wa maradhi hayo kuwaambukiza watu
wengine ikiwa ni sehemu ya kulipiza kisasi” Alisema
Aidha Bi. Valeria amewaomba wanajamii kuwajali na kuwatunza watu
wanaoishi na maradhi ya kuambukiza ili kuwaondoshea hali simanzi, hasira,
visasi na upweke.
“Niwaombe sana mukawaelimishe wananchi juu ya umuhimu wa
kuwajali na kuwatunza watu wanaoishi na maradhi ya kuambukiza kwasababu kitendo
cha kumnyanyapaa mtu kinaongoza ugonjwa, simanzi, hasira, kisasi na upweke na
ndio maana baadhi ya wahisiwa wa maradhi hayo hufikia pahala wakachukuwa hatua
mbaya ikiwemo kulipiza kisasi kwa kuwaambukiza wengine au kujinyonga” Bi.
Valeria
Akiwasilisha mada juu ya maradhi ya Kfua Kikuu, mratibu wa
Kifua Kikuu na Ukoma Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Said Khamis Ahmada,
amesema inakisiwa kuwa takribani Wazanzibari 124 kati ya Wazanzibari laki moja wanahisiwa
kuugua kifua kikuu sawa na wahisiwa 1,612 kila mwaka.
“Kifua kikuu ni ugonjwa magonjwa kumi yanayosababisha vifo
vingi duniani, inakisiwa kuwa watu milioni 10 wameugua TB na milioni 1.5
wamefariki kwa ugonjwa kifua kikuu katika mwaka 2020 duniani kote” Said Khamis
Ahmada
“Takwimu za maradhi ya Kifua Kikuu kwa 2020-2021 za Wilaya
zinaonesha Wilaya ya Mjini Magharibi B ndio Mkoa unaongoza kwa wahisiwa wa
kifua kikuu kwa kuwa na wahisiwa 163 mwaka 2021 kutoka wahisiwa 124 mwaka 2021
ukifuatiwa na Wilaya ya Wete Pemba kwa kuwa na wahisiwa 140 mwaka 2020 kutoka
wahisiwa 105 mwaka 2021” Said Khamis Ahmada
“Kwa upande wa takwimu za ugonjwa wa Kifua Kikuu Zanzibar
kutoka mwaka 2017 hadi 2021 zinaonesha takriban watu 1090 wamehisiwa kuwa na
maradhi ya Kifua Kikuu kutoka watu 948 mwaka 2017” Alisema

Kwa upande wake, mratibu wa Kifua Kikuu na Ukoma kanda ya
Pemba Hamad Omar Hamad, amesema takwimu
zionanesha jumla ya Wazanzibari 7,524 na virusi vya Ukimwi kwa mwaka 2019,
ambapo idadi ya maambukizi jumla katika jamii ni sawa na asilimia 0.4.
Ameongeza kuwa, kwa mujibu wa takwimu wanawake ndio
wanaoongoza kwa maambukizi ya virusi vya Ukimwi Kuliko wanaume Visiwani
Zanzibar.
“Wagonjwa 3 wa mwanzo walioambukizwa virusi vya Ukimwi
Zanzibar waligunduliwa mwaka 1986, katika hospiati ya Mnazi Mmoja, takwimu
zinaonesha idadi ya maambukizi kwenye jamii ni asilimia 0.4 hadi sasa ambapo
jumla ya watu 7524 wameambukizwa VVU mwaka 2019 huku takwimu zikionesha
wanawake kuwa wengi ikilinganishwa na wanaume katika maambukizi hayo” Hamad
Omar Hamad

Abdi Suleimani ni mwandishi wa gazeti la Zanzibar leo Kisiwani
Pemba, amewaomba watendaji wa wizara ya afya kisiwani Pemba kuandaa program
maalumu za kutoa mafunzo kwa vijana hususan bodaboda ili kuwanusuru vijana hao.
“Licha ya mafunzo haya kwa waandishi wa habari lakini bado muna
jukumu kubwa la kuendelea kutoa elimu kwa vijana hususan vijana wa bodboda wa
Machomanne wameharibika sana kimaadili na inadaiwa kuwa kuna baadhi ya ndugu
zetu wanatoka Tanzania bara kuja Pemba kwa ajili ya kufanya biashara ya kuuza
miili yao na inasemekana wateja wao wakubwa ni vijana hususan bodaboda sasa
musipoliangalia hili kwa macho mawili tunaweza kuja kuwapoteza vijana wengi
sana hapo baadae” Abdi Suleiman
Wa Pili kutoka kulia ni Mwandishi wa Habari wa Gazeti la Zanzibar Kisiwani Pemba Leo Abdi Suleiman akiwa na Mwandishi mwenzake Habiba Zarali Rukuni.
Akiitoalea ufafanuzi hoja hiyo, Mratibu wa Kitengo Shirikishi
ZIHHTLP Pemba, Khamis Hamad Ali, amesema Wizara ya Afya Zanzibar imeandaa
utaratibu wa kukutana na wananchi mbali mbali wakiwemo Vijana ili kutoa elimu
juu ya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi ikiwemo namna ya kujikinga na maambukizi
sambamba na kupima afya zao kwa hiari.
“Kwanza ahsante sana kwa taarifa pili niseme kuwa Wizara ya
Afya Zanzibar tumekuwa na utaratibu endelevu wa kukutana na wananchi mbali
mbali wakiwemo Vijana katika kutoa elimu ya kujikinga maambukizi ya VVU pamoja
na kupima afya zao kwa hiari na ukweli ni kwamba vijana wengi sasa hivi wana
taaluma ya kutosha kuhusu VVU na kutambua umuhimu wa kucheki afya zao mara kwa
mara” Mratibu ZIHHTLP
Nao Waandishi walioshiriki katika hafla hiyo wameahidi
kuyafanyia kazi mafunzo hayo kwa kuandika habari zitakazo waelimisha wananchi
kuhusu athari hasi za kuwanyanyapaa wahisiwa wa maradhi ya kuambukiza ikiwemo
Kifua Kikuu, Uviko19 pamoja Ukimwi.
Mafunzo hayo ya siku moja yalikuwa na lengo la kutoa elimu
kwa waandishi wa habari Kisiwani Pemba juu ya athari ya kuwanyanyapaa wahisiwa
wa maradhi ya kuambukiza ikiwemo Kifua Kikuu, Uviko19 pamoja na Ukimwi.