Mwanamke mmoja nchini Misri anayefahamika kwa jina Amani Abdul-Karim Al-Gazzar mwenye umri wa miaka 19, ambaye ni mwanafunzi wa elimu ya viungo ameuawa kwa kupigwa risasi baada ya kukataa ombi la kuolewa na mwanamme aliyemzidi umri.
Mwanafunzi huyo alipigwa risasi mgongoni
nje ya nyumba yao baada tu ya yeye familia yake kukataa pendekezo la ndoa
kutoka kwa Ahmed Abou Ameirah mwenye umri wa miaka 29, ambaye pia alijipiga
risasi muda mchache baada shambulio hilo siku ya Jumamosi Septemba 03, 2022.
Taarifa kutoka jeshi la Polisi
zimeeleza kuwa Ahmed alimuua Amani kwa hasira baada ya yeye na familia yake
kukataa pendekezo lake la ndoa kabla ya kukimbia eneo la tukio katika kijiji
cha Takh Tanbisha karibu na Mji Mkuu wa Misri, Cairo.
Kabla ya kujitoa uhai, mwanamme huyo
aliwahi kurekodi video fupi akisema amekuwa akiishi kwa ajili ya mwanamke huyo,
hivyo kukataliwa kwake kumemfanya ajisikie vibaya na hivyo lazima atalipiza
kisasi.
Mauaji hayo ya kutisha yanakuja
wakati Misri ikikabiliana na viwango vya uhalifu wa kikatili vinavyoongezeka
unaowalenga wanawake, huku kukiwa na kesi nyingi za juu zinazohusisha wanawake
ambao walikataa kushawishiwa na wanaume.
Tukio hilo la mauaji linafuatiwa na
mauaji ya Naira Ashraf ambaye aliuawa nje ya chuo kikuu cha Kaskazini mwa Misri
alipokuwa akielekea kwenye mitihani yake ya mwisho baada ya kukataa mapendekezo
kadhaa ya ndoa kwa muuaji wake.