RIPOTI YA ‘CAG’ YAMNG’OA KAMISHNA MAKARANI ZAECA.
Aliyekuwa Mkuu wa Mamlaka ya kuzuia
Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar ‘ZAECA’ Ahmed Khamis Makarani, amejiuzulu baada
ya ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa hesabu za Serikali ‘CAG’ kuwasilisha ripoti
kwa Mhe. Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ripoti iliyoonesha upotevu
wa mamilioni ya fedha.
Taarifa ya kujiuzulu kwa Kamishna
Makarani, imetolewa na mkurugenzi wa Mawasiliano ya Ikulu, Charles Hillary
kupitia taarifa iliyotolewa na vyombo vya habari leo Septemba 02\2022.
“Rais wa Zanzibar amekubali barua ya
kujiuzulu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar,
Ahmed Khamis Makarani”
Imesema taarifa hiyo ikieleza kuwa ni
hatua inayofuatia kauli ya Rais Dk. Mwinyi kutaka ZAECA kujitathmini.
Rais DK. Mwinyi aliwataka watendaji wa ZAECA kujitathmini kutokana na ripoti ya CAG kuonesha upotevu mkubwa wa fedha wakati akihutubia hadhara ya viongozi mbali mbali baada ya kupokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa Zanzibar ‘CAG’ ya Mwaka 2020/2021.
Ripoti iyo imeeleza kasoro nyingi za
matumizi ya fedha za Serikali zinazosababisha ubadhirfu wa fedha wa mamilioni
ya fedha.
Dk. Mwinyi akionesha kukerwa na
ufisadi Serikalini alisema anashangazwa kukuta matatizo hayo yanajirudia na
hakuna hata mtuhumiwa mmoja aliyefikishwa kwenye vyombo vya Sheria.
Alisema anashangaa kwamba hakuna kesi
hata moja iliyopelekwa mahakamani wakati ofisi yake imekabidhi kwa ZAECA ripoti
yenye maelezo thabiti ya namna ufisadi ulivyofanyika na wahusika kutajwa na
baadhi yao ukukiri na kurudisha fedha.
“Hatuwezi kuendelea hivi wizi kila
mahali na hakuna kesi iliyopelekwa mahakamani kwa namna hii inabidi ZAECA
mujitathmini hatuwatendei haki wananchi” alisema Dk. Mwinyi baada ya kusikiliza
maelezo ya ripoti ya masaa manne mfululizo kutoka kwa CAG Dk. Othman Abbas Ali akieleza
namna mabilioni ya fedha yalivyopotea huku wahusika wakikosa majibu.
Makarani ambaye ni afisa mwandamizi
wa Jeshi la Polisi Tanzania mwenye cheo cha kamishna msaidizi ‘Assistant Commissioner of Police' (ACP) ambapo kabla ya kuteuliwa kushika nafasi hiyo
alikuwa Kamanda wa Polisi kamishna msaidizi wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba.
Chanzo. Mwanahalisi.