Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Alhaj Othman Masoud Othman, amesema kuwa kushindwa kutumia vyema hazina kubwa iliyopo visiwani hapa, ni katika mambo yanayodhoofisha juhudi za kujenga ustawi bora wa Nchi.
Alhaj Othman ameyasema hayo leo, hatika salamu zake kwa waumini wa Kiislamu, mara tu baada ya Swala ya Ijumaa, huko Kinyasini Kisongoni, Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Amesema miongoni mwa hazina hiyo na raslimali muhimu, ambazo zitapelekea majuto, hasa baada ya kuondoka duniani, ni kwamba Zanzibar imebarikiwa kuwa ni Visiwa vya Watu wamoja ambao fungamano la maisha yao pia linatokana na raslimali ya umoja huo.
Mheshimiwa Alhaj Othman amefahamisha kuwa, kwa kiasi kikubwa, kinachopelekea Wazanzibari kuwa wamoja ni kutokana na thamani ya udugu wao wa nasaba, pamoja na mila na silka imara zilizoasisiwa na Dini, ambazo tangu asili zinawaongoza wao kuwa wamoja na si vinginevyo.
“Nataka niunganishe pale ambapo amemalizia Khatib wa Swala hii, watu wote wa Nchi hii ni wamoja, ambao mila na utamaduni wao, pia unawahamasisha wabaki ni wenye kushikamana na kuishi pamoja, kuendelea kujenga jamii iliyoneemeshwa kama zamani”, ameeleza Alhaj Othman.
Mheshimiwa Alhaj Othman amewakumbusha waumini, juu ya haja ya kuendeleza mila hizo, ili kulinda mshikamano wao uliotokana na udugu wa nasabu, mila na desturi imara zilizofungamana, akisema jambo hilo ni wajibu kidini na kijamii.
Hivyo amewahimiza waumini pamoja na wananchi wote kuwa wasikivu, na wenye kufuata mawaidha mema wanayoyapata katika Misikiti au majukwaa yoyote mema, ili kuhakikisha ustawi bora wa jamii ya watu wamoja.
Akisoma Khutba Mbili za Swala hiyo, Khatwiib Sheikh Is-haka Vuai Kidawa, amewakumbusha Waislamu, wajibu wa kufuata na kutekeleza mafunzo ya Dini, na kwamba kila mmoja atalipwa kwa mujibu wa mambo mema au mabaya aliyoyatenda katika maisha ya dunia.
Sheikh Is-haka amewahimiza Waislamu umuhimu wa kupendana, kuhurumiana na kusaidiana, ili kuijenga jamii ya watu waliopewa neema za kuendelea, kama ambavyo Misingi Mitukufu ya Dini, imefahamisha kutekeleza hayo.
Katika Ibada, hiyo Viongozi mbali mbali mbali wa Serikali, Dini na Jamii wamehudhuria, wakiwemo Mkurugenzi wa Baraza la Mji, Wilaya ya Kaskazini B, Nd. Abrahman Ali Mukhtar; na Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo-Zanzibar, Mhe. Salim Bimani.
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
Septemba 30, 2022