TUSIMAMIE HAKI ILI KULETA MAENDELEO KATIKA NCHI - MHE. OTHMAN

Hassan Msellem
0

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama cha ACT-Wazalendo Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, amesema kukosekana kwa mfumo wa haki unaopelekea kuwapata viongozi imara na wanaostahiki kuiongoza Nchi, ni moja ya mambo yanayokwamisha juhudi za wananchi kuyafikia maendeleo ya kweli. 


Mhe. Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ameyasema hayo leo kwa nyakati tofauti, katika mwendelezo wa ziara yake ya ujenzi na uimarishaji wa Chama, alipotembelea Majimbo ya Chaani na Mkwajuni, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Amesema kuwa mfumo huo ni ule ambao unatokana na uwepo wa taasisi imara zinazoweza kuasisi utaratibu wa kuwapata viongozi wanaoridhiwa na umma na kupata ridhaa ya kuiongoza Nchi, kwa kufuata misingi ya haki, heshima na uadilifu.

Mheshimiwa Othman amezitaja taasisi hizo kuwa ni pamoja na zile zinazoaminika katika kulinda kwa uadilifu raslimali, mali za umma na haki za wananchi wote bila ya ubaguzi, zikiwemo mamlaka za kusimamia sheria na Tume za Uchaguzi. 

Akiongea na viongozi, wanachama na wafuasi wa ACT-Wazalendo katika Majimbo hayo, Mheshimiwa Othman ameeleza dhamira ya Chama hicho kuendeleza harakati ambazo msingi wake ni upatikanaji wa taasisi hizo ambazo hatimaye zitasimamia juhudi na matumaini ya umma, katika kufikia Zanzibar wanayoihitaji na maendeleo wayatakayo.

“Hatutoweza kuitekeleza dhamira hiyo bila ya kushikamana na kuungamkono kwa pamoja juhudi za kujenga na kuimarisha Chama imara ili hatimaye tuweze kufikia Zanzibar tuitakayo, yenye mamlaka kamili na maendeleo ya kweli ambayo waasisi wetu waliipigania kwa dhati,” amefahamisha Mheshimiwa Othman.

Aidha, Mheshimiwa Othman ameeleza kwamba yeye na viongozi wenzake wanaelewa machungu na maumivu ambayo waliyapata na wanaendelea kuyapata wananchi, yakiwemo maonevu na ukali wa maisha, bali wasikate tamaa kwani safari ya kupigania Zanzibar yenye maendeleo ya kweli inaendelea.

Akiongelea juu ya changamoto mbali mbali zilizowasilishwa na wananchi, zikiwemo uporwaji wa ardhi na mashamba ya watu wa Kijiji cha Kandwi, Jimbo la Chaani, Wilaya ya Kaskazini A Unguja, Mheshimiwa Othman ameahidi kwamba dhulma ya aina yoyote haiwezi kupuuzwa, na kwamba lazima kuwepo na utaratibu ambao yeye binafsi atausimamia kuhakikisha haki inatendeka.

Kwa upande wake, Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Bw. Salim Bimani, ametoa wito kwa wananchi kuepuka kukata tamaa katika kuungamkono juhudi za kuipigania Zanzibar yenye mamlaka kamili, ambayo ndiyo njia pekee ya kufanikisha matumaini ya Wazanzibari katika kujiletea maendeleo ya kweli wakiwa huru.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT-Wazalendo, Bw. Ismail Jussa Ladhu.

Naye, Mjumbe wa Kamati Kuu ya ACT-Wazalendo, Bw. Ismail Jussa Ladhu, akikumbusha madhara na mateso aliyoyapata yeye binafsi yakiwemo kupigwa na kujeruhiwa vibaya, wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020, amewahimiza vijana kuepuka kukata tamaa na kuzidisha ari ya kumuungamkono Mheshimiwa Othman, ambaye ni Mrithi wa Muasisi wa Uongozi wa Chama hicho na harakati za kupigania Mamlaka Kamili ya Zanzibar, Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad.

"Katika hali hii ya maisha magumu na umasikini uliokithiri kuna sababu yoyote ya wewe kijana kuvunjika moyo na kuwacha kuendelea kuungamkono harakati za kuipigania Zanziibar yenye Mamlaka kamili," amehoji Jussa.

Katika salamu zake, Katibu wa Oganaizesheni wa Chama hicho, Ndugu Omar Ali Shehe, ameeleza mafanikio wanayoendelea kuyapata katika utekelezaji wa dhamira yao, ikiwemo uungwajimkono na umma mkubwa, sambamba na mwitikio wa wanachama wengi, katika kufanikisha Sera yao Mpya ya ACT-Kiganjanii.

Katibu wa Oganaizesheni wa Chama hicho, Ndugu Omar Ali Shehe.

Viongozi mbali mbali na Watendaji wa Chama hicho wamejumuika katika ziara hiyo, wakiwemo Wenyeviti na Makatibu wa Mikoa, Wajumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya ACT-Wazalendo.


Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

 

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top