Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi amehimiza haja ya ushiriki wa wanawake na vijana katika shughuli mbali mbali za biashara, ili kuhamasisha maendeleo ya Bara la Afrika.
Mheshimiwa Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo wakati wa Hafla ya Ufungaji wa Mkutano wa Kimataifa wa Wanawake na Vijana katika Biashara, chini ya Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika, iliyofanyika katika Ukumbi wa Mwalimu Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam, Tanzania.
Katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Othman Masoud Othman, Dkt. Mwinyi amesema kuwa kushiriki pamoja na mchango wa wanawake na vijana kwenye biashara, kutawezesha kuzitumia ipasavyo fursa ziliopo ndani ya Bara hili tajiri la raslimali, na hatimaye kupelekea Afrika yenye maendeleo.
Akiendelea kuhamasisha haja ya mashirikiano miongoni mwa wadau wote, huku akitumia nafasi hiyo kuwaomba wanawake na vijana wa Afrika kuhakikisha wanatumia vyema fursa zinazopatikana kwa manufaa ya Waafrika wote, Mhe. Dokta Mwinyi amesema, " wito wangu, tuendelee kushirikiana zaidi ili kwa pamoja tuweze kuifikia Afrika tuitakayo yenye umoja, amani na maendeleo".
Aidha, Mhe. Dokta Mwinyi ameeleza kwamba mwenendo wa kupendelea bidhaa za ndani utasaidia kutimiza malengo ya Biashara chini ya Mkataba wa Eneo huru la Biashara la Afrika, sambamba na kukuza Viwanda Barani humu, kama sehemu ya jitihada za kujiletea wenyewe maendeleo na hatimaye kujikwamua kiuchumi.
Ametilia mkazo utekelezaji wa Kaulimbiu ya Mkutano huo, ambayo insema, "Wanawake na Vijana ni Injini ya Biashara chini ya Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika".
Aidha amesema kwamba Mkutano na Maonesho ya Biashara yaliyofanyika yametoa elimu kubwa na kutengeneza fursa pana kwa washiriki hao kubadilishana uzoefu na taarifa muhimu za kibiashara na kuwataka kuendelea kubadilishana uzoefu ili kuzitumia vyema fursa za kibiashara zilizopo katika soko huru la Afrika.
Amesema mkutano huo pia umetoa fursa ya kuwepo mjadala maalum na kutoa mapendekezo kuhusu Itifaki ya Wanawake na Vijana katika Biashara chini ya Mkataba wa Eneo Huru la Biashara la Afrika.
Naye Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia wazee na Watoto Zanzibar Mhe. Riziki Pembe Juma, amesema kwamba sera za kiuchumi na biashara zinazotungwa na Serikali za Afrika hivi sasa zinajielekeza zaidi kuunga mkono jitihada za ushiriki mpana wa wanawake na vijana katika kukuza uchumi kupitia shughuli za kibishara.
Kwa Upande wake Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Mhe. Omar Said Shaaban, amesema kwamba changamoto kubwa iliyopo katika Sekta ya Biashara kwa vijana na wanawake wa Afrika, sio sera na sheria bali ni namna ya kuzitafsiri katika kuimarisha biashara na kuendeleza ukuaji wa uchumi na maendeleo.
Hivyo, amepongeza mapendekezo na mijadala mbali mbali ya Mkutano huo yanayolenga kukuza ushiriki wa vijana na wanawake katika biashara, hali ambayo ni kinyume na utaratibu uliozoeleka kwa viongozi kujifungia pekee na kuamua mipango juu ya uendeshaji wa makundi hayo muhimu ya jamii.
Naye Katibu Mtendaji wa Sekretarieti wa Eneo Huru la Biashara Afrika Bwana Mamkele Mene, amesema kwamba Mkutano huo uliofanyika kwa ufanisi ni muhimu sana, ambapo mijadala yake italenga katika kupatikana suluhisho la changamoto mbali mbali za kibiashara zinazojitokeza hasa kwa vijana na wanawake, Barani Afrika.
Akisifia juhudi zinazotekelezwa pamoja na mafanikio ya Wakala wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA), Bw. Mene amesisitiza haja ya ushirikishwaji wa wadau wote akisema, "Afrika itajengwa na Waafrika wenyewe".
Mkutano huo wa Siku Tatu, ambao umehusisha mada, maazimio na mijadala mbali mbali, na ambao ulifunguliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan, mnamo Septemba 12, 2022 umewajumuisha Viongozi, Wajasiriamali, Mabalozi, Wakuu wa Mashirika ya Kitaifa na Kimataifa, Vijana na Wanawake zaidi ya 500 sambamba na Waoneshaji wa Maonyesho ya Biashara kutoka Mataifa ya Afrika.
Kitengo cha Habari
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar
Septemba 14, 2022.