Mnamo tarehe 02/10/2022 majira ya saa moja na nusu jioni katika kata ya kolandoto manispaa ya shinyanga Mtu mmoja asiyefahamika na anayesadikika kuwa na matatizo ya akili alishambiliwa kwa kupigwa kisha kuchomwa moto na wananchi wenye hasira kali mara baada ya mtu huyo kufanya mauaji ya watu wawili waliofahamika kwa majina ya Nikolaus Leornad (43) na Badimartha Merrikiadi (33).
Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa shinyanga ACP. Janeth Magomi amesema mtu huyo asiyefahamika anayekadiliwa kuwa na umri kati miaka 32 hadi 35, alikuwa akionesha tabia ambazo si za kawaida kama kung’ata watu masikio na kupiga watu wa eneo hilo waliona kama ni mwenye matatizo ya akili,na mara baada ya kukithiri kwa vitendo hivyo mtaa hapo ndipo watu wa eneo hilo walichukua jukumu la kutaka kumkamata.
“Majira ya saa 12 za jioni jamii ya eneo hilo walianza kujikusanya ili waweze kumkamata ndipo mtu huyo alipoanza kukimbia na kuokota kipande cha nondo pamoja na shoka, alipokuwa akikimbizwa na kuingia kwenye nyumba ambayo ndani ya hiyo nyumba kulikua na watu watatu ambao ni baba, mama na rafiki wa mama wa familia hiyo”.
Ndipo kijana huyo alipoanza kumkatakata baba wa familia hiyo na kisha kumkatakata rafiki wa mama wa familia hiyo, mama wa familia hiyo alifanikiwa kukimbia, mama huyo amelazwa hospitali ya rufaa mkoa wa shinyanga, alipata mshtuko baada ya kushuhudia mume wake akiuawa”, amesema Magomi.
Diwani wa Kolandoto Mussa Andrew, amesema baada ya kupokea taarifa alifika eneo la tukio na kumkutana Mtu huyo akiwa bado ndani ya nyumba hiyo, akapiga simu kuomba msaada Polisi, lakini wananchi wenye hasira kali walifanikiwa kumtoa nje na kisha kuanza kumkimbiza, walifanikiwa kumkamata na kisha kuanza kumpiga kwa mawe na baadae kumchoma moto.
Naye Mganga Mkuu wa Hospitali ya Kolandoto Dk. Joseph Wallace, amethibitisha kupokea miili ya marehemu watatu akiwamo na kijana ambaye aliuawa na wananchi, pamoja na majeruhi watatu huku mmoja akipewa rufaa ya kwenda Bugando jijini Mwanza kwa matibabu zaidi lakini naye amepoteza maisha jioni ya leo.