ADAIWA KUJINYONGA KWA MADAI YA KUNYIMWA MSHAHARA WAKE

0

 Ofisa Muuguzi (II) wa Hospitali ya Taifa Muhimbili- Mloganzila, Dar es Salaam, Sarwat Soluwo amedaiwa kujinyonga hadi kufa kwa kilichodaiwa mateso aliyopitia baada ya kusimamishiwa mshahara na uongozi wa hospitali hiyo.

PICHA KUTOKA MAKTABA HAIHUSIANI NA TUKIO HALISI

Taarifa za ndani ya hospitali hiyo zinaeleza Sarwat alisitishiwa mshahara kwa miezi michache iliyopita kutokana na tabia ya ulevi huku akihitajika kuendelea na kazi bila ya mshahara.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alithibitisha kutokea kwa tukio la kujinyonga kwa kijana huyo na kusema uchunguzi unaendelea.


Kwa mujibu wa taarifa, baada ya kufanya kazi kwa muda bila mshahara, adhabu hiyo ilimuathiri na kugeuka ombaomba hospitalini hapo, ili apate fedha za kula pamoja na za kumuwezesha kufika kazini.

“Hali ilizidi kuwa ngumu kwake, akaanza kuuza vyombo vya ndani, ili apate kula na nauli, kuna kochi alinunua fedha nyingi aliuza Sh60,000 kwa sababu ya ugumu wa maisha na alizidisha unywaji wa pombe zaidi.

“Baada ya kulewa kuna watu walimdhuru akaletwa hospitali, alivyorudi nyumbani kwake hali ile ikamkwaza akachukua uamuzi wa kujinyonga,” alidai mfanyakazi mwenzake.

Shuhuda huyo ambaye hakutaka jina lake litajwe alidai Sarwat kabla ya kuchukua hatua hiyo, aliweka picha ya mpenzi wake kwenye mtandao wake wa kijamii huku akibadilisha muonekano wa juu akiweka kiatu.

Shuhuda huyo alidai uongozi wa hospitali hiyo umekuwa ukiwanyima haki wafanyakazi kwa kuwanyima mishahara, kutoa adhabu bila kufuata utaratibu.

Hata hivyo, Mwananchi lilizungumza na Ofisa Uhusiano wa Muhimbili, Aminieli Eligeisha aliyesema “ni kweli marehemu alikuwa mfanyakazi wetu alifariki jana (juzi) nyumbani kwake, sababu zilizopelekea kifo chake na mengine yanayosemwa polisi wanachunguza na watatupatia majibu.


“Taratibu zote za kiutawala zinaendelea kufanyika kuhakikisha tunamuaga na kwenda kumpumzisha nyumbani kwao Arusha. Kesho (leo) asubuhi itafanyika ibada Mloganzila.”

Said Joseph, dereva bodaboda eneo la Chama alidai rafiki yake huyo kabla ya umauti alichukuliwa na gari maalumu la wagonjwa na kwenda kufungiwa kwenye vyumba vya wagonjwa wa akili kwenye hospitali ya Mloganzila.

Fatma Juma, mwanamke aliyekuwa akiishi na Sarwat alisema jambo pekee alilomshirikisha ni la ndugu zake kutaka kumhamisha kituo cha kazi.

Hata hivyo, alisema sababu za ndugu hao kutaka kumhamisha hakumueleza, lakini amekuwa akipokea simu za vitisho kutoka kwa ndugu wa mwanaume huyo.

“Kabla ya kufariki kwa mume wangu nilipigiwa simu na ndugu yake mmoja akaniambia nimwambie mume wangu aniambie maneno ya mwisho, sikuelewa mpaka tukio hili lilipotokea,” alidai Fatma.

Akizungumzia tukio sakata la mumewe kubebwa na gari la wagonjwa, alikiri tukio hilo kuwepo na bado hajafahamu mambo yaliyoendelea mpaka kilipotokea kifo.


Chanzo;Mwananchi

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

 

 

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top