Jamaa huyo alikuwa akiishi katika makao ya watu maskini ya Kithyoko Mercy katika eneo la Masinga.
Mwamali Muthiani alifikishwa katika makao hayo baada ya kukosa kutambua familia yake kufuatia ajali mbaya iliyopelekea majeraha kichwani na kulazwa katika hospitali ya kitaifa ya Kenyatta. Hii iliharibu kumbukumbu yake.
Mwanamume huyo alikuwa amekaa ndani ya nyumba hiyo kwa zaidi ya miaka minne sasa, katika kipindi hicho alianza kurejesha kumbukumbu zake na aliweza kutamka majina ya wanafamilia yake na hata kuweza kutaja kijiji na eneo lake.
Sista Mary Musembi, mtawa wa Kikatoliki anayesimamia Kithyoko Mercy Home ya wasio na makao alichukua hatua ya kuwasiliana na chifu wa eneo hilo na hivyo ndivyo wanafamilia wake walivyofuatiliwa.
"Alipoanza kutaja majina ya jamaa wa familia yake na kijiji chake, niliwasiliana na chifu wa eneo hilo na tukaweza kuungana na familia yake," alisema Musembi.
Aliongeza kuwa jama wake hawakuamini kuwa jamaa yao alikuwa hai hadi alipofika nyumbani na kuungana nao.
Mamake, Monica Muthiani, alijawa na furaha alisema kwamba alikuwa amepoteza matumaini ya kupata mwanawe wa pili lakini kwa neema ya Mungu hatimaye wamempata. Alimshukuru dada Mary Musembi kwa kumtunza vyema akiwa katika makao hayo.
Dadake Ann Twili alishindwa kuzuia machozi ya furaha baada ya kumwona kakake ambaye alikuwa ametoweka kwa zaidi ya miaka saba. Kulingana naye, walikuwa wamemtafuta kaka yao kila mahali ikiwa ni pamoja na katika vyumba vya kuhifadhia maiti lakini juhudi zao hazikuzaa matunda.
Maombi yao hata hivyo yalizaa matunda baada ya kupokea simu kutoka makao ya Kithyoko Mercy kusema kuwa kaka yao alikuwa hai.
Mkurugenzi wa Huduma za Kijamii katika Hospitali ya kitaifa ya Kenyatta Kadie Kerwang aliwataka jamaa ambao hawawezi kuwatafuta wapendwa wao kuwasiliana na hospitali hiyo, kwani kuna watu wengine wengi, ambao wanafamilia wao hawawezi kufuatiliwa, huku 12 wakihifadhiwa katika nyumba ya wasio na makao.