Hatua hiyo imekuja ikiwa ni siku moja baada ya kikosi kazi kukabidhi ripoti yenye mapendekezo 18 kwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza jana mkoani Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa chama hicho, John Mnyika, alisema katika uchambuzi wao wa awali kuhusu mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa, alisema jambo hilo lilitakiwa kutolewa uamuzi wa haraka.
“CHADEMA kinatoa wito kwa serikali kujitokeza bila kusubiri marekebisho ya Kanuni ya Vyama vya Siasa mwaka 2019, marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa, iondoe zuio waliloliita hili haramu la mikutano ya hadhara,” alisema.
Mnyika alisema katika jambo hilo wanasisitiza kuwa azimio lililotolewa na Kamati Kuu ya CHADEMA Septemba 17 na 19 mwaka huu, pamoja na kutoa wito wa kuondoa zuio hilo, ilitoa maelekezo kwa ngazi zote za chama kuendelea na maandalizi ya mikutano ya hadhara katika tarehe ambayo itatangazwa.
“Chama kitaendelea kutimiza haki ya kikatiba na kisheria kufanya mikutano ya hadhara kwa mujibu wa kifungu cha 11 cha Sheria ya Vyama vya Siasa na vifungu vya 43 mpaka 46 vya Sheria ya Jeshi la Polisi,” alisema.
Katibu Mkuu huyo alisema jambo hilo lilikuwa rahisi ambalo lilitakiwa kutolewa uamuzi kwa mujibu wa vifungu hivyo vya sheria.
Kuhusu mchakato wa katiba mpya, Mnyika alisema Mwenyekiti wa kikosi kazi alieleza kuwa walipokea maoni ya aina mbili, kundi lililosema hakuna sababu ya kuandikwa kwa katiba mpya ila kama kuna marekebisho yafanyike na la pili la maoni yaliyogawanyika makundi matano.
Alisema mwenyekiti aliligawa kundi la pili linalotaka katiba mpya katika makundi madogo matano, lakini hakutoa sababu za msingi za kuachana na kundi ambalo yeye alilitaja ni la tatu lililosema mchakato huo uendelee kwa kuuondoa ulikokwamia kuanzia rasimu ya pili ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba maarufu ‘Tume ya Jaji Warioba’.
Alisema mwenyekiti hakutoa sababu za msingi, badala yake akarukia na kusema kikosi kazi kimekubaliana na maoni yanayosema, liundwe jopo la wataalam ambalo litaandaa rasimu ya tatu ya katiba na kupeleka bungeni kupitishwa kabla ya kupigiwa kura ya maoni.
“Hapa ndipo ilipo dhamira mbaya na nia ovu ya kikosi kazi. Bunge la sasa na umma unajua lilivyopatikana katika uporaji wa ridhaa ya wananchi ulioitwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
“Bunge hilo sasa ndo eti linakwenda kukabidhiwa kazi tukufu na kazi takatifu kupitia rasimu ya tatu ya katiba, Bunge la namna hii lenye hodhi ya chama kimoja likiruhusiwa kufanya kazi hii litakwenda kuharibu zaidi.
“Kitakachotoka kitakuwa kibaya kuliko rasimu ya Jaji Warioba au Katiba Pendekezwa, kitakuwa kibaya zaidi na sumu ya kuua mchakato wa katiba mpya au kuuvuruga kupindukia mchakato huo,” alisema.
Mnyika alisema CHADEMA ilitarajia kikosi kazi kingekuja na mapendekezo ya ama kutengenezwe chombo cha kitaifa chenye kuundwa na wawakilishi wa wananchi kutoka makundi mbalimbali au wajumbe wa kuchaguliwa, kwa minajili ya kufanya kazi ya kutunga katiba mpya.
Alisema mapendekezo ya kikosi kazi hicho, yangekuwa na mantiki, kama yasingelihusisha Bunge katika kupitisha rasimu ya tatu ya katiba mpya.
Pia alisema hatua iliyofanywa ya pili ya kuhusisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na Sheria ya Kura ya Maoni ilipaswa iwe hatua ya kwanza na ingepelekwa Bunge la mwezi Novemba ili kukwamua na kukamilisha mabadiliko ya katiba.
Pia alisema hatua iliyofanywa kwanza na kikosi kazi hicho ya mjadala wa kitaifa wa kupata muafaka katika masuala ya msingi, ingekuwa ndiyo hatua ya pili, kwa muswada wa sheria kupelekwa bungeni ili kuweka utaratibu wana namna gani ya kuendesha mjadala wa kitaifa vyombo vipi vitumike.
Mnyika alisema hatua waliyoitaja ni ya tatu ya kuundwa kwa jopo la wataalam, ingekuwa ni ya nne ambayo ingehusisha kuweka katika maandishi huo muafaka wa kitaifa kutafsiri kutoka katika lugha ya kisiasa, lugha ya kijamii na ya kiuchumi na kuwa lugha ya kisheria.
Alisema utaratibu uliopendekezwa na kikosi kazi ni mbovu usiokuwa na ratiba, utaratibu na muundo muafaka wa kujenga muafaka wa kitaifa.
Alisema CHADEMA itaendelea kulinda maoni ya wananchi kuhusu haja ya katiba mpya.
Kuhusu tume huru ya uchaguzi, chama hicho kilisema kuwa, walitarajia kingekuja na mapendekezo yaliyochambua Mkataba wa Afrika wa masuala ya demokrasia, utawala na uchaguzi ambao umeweka misingi, tume inapaswa iundwe vipi.
“Wangekuja na utafiti, na utafiti tayari Tume ya Jaji Warioba ilishaufanya, wangeurejea kitabu cha utafiti wangeangalia nchi nyingine zenye miundo bora ya tume ya uchaguzi, wangekuja na mapendekezo ambayo yeyote angeona angesema hii ni Tume Huru ya Uchaguzi.
Alisema ili waendelee na mchakato wa katiba ulipokwamia, rasimu ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ndipo pawe pa kuanzia.
Kuhusu pendekezo la sheria ya vyama vya siasa ifanyiwe marekebisho ili kulipatia baraza la vyama lililoundwa na vyama vyenyewe mamlaka ya kushughulia uvunjifu wa maadili ya vyama kupitia kamati ya maadili, Mnyika alisema lina dhamira ya kuthibiti vyama vikuu vya upinzani hasa CHADEMA.
Mnyika alisema CHADEMA kinaitaka serikali iweke wazi gharama ambazo kikosi kazi imezitumia.