ASKOFU Mkuu mstaafu wa Kanisa la Anglikana Tanzania, Dk Donald Mtetemela, amewataka viongozi wa dini nchini kujiepusha na kauli na viendo vitakavyopandikiza chuki na uchochezi kwa waumini wao dhidi ya serikali na dini nyingine.
Askofu Mtetemela ametoa kauli hiyo jana, wakati wa ibada ya kumweka wakfu na kumsimika Kasisi Noel Mbawala kuwa Askofu wa kwanza wa Kanisa la Upendo wa Kristo Masihi (KIUMA), lililopo Kijiji cha Milonde kata ya Matemanga, Wilaya ya Tunduru.
Ibada hiyo imeongozwa na Mhashamu Baba Askofu Mkuu wa Kanisa la Anglikana Tanzania na Dayosisi ya Tanga, Maimba Mndolwa, kwa niaba ya Makanisa ya Jumuiya ya Kikiristo Tanzania (CCT), baada ya kanisa hilo kujiunga rasmi na jumuiya hiyo.
Pia Dk Mtetemela, amewataka viongozi wa dini hapa nchini, kushirikiana na kuheshimu mamlaka za serikali, ili kuendelea kutunza amani na mshikamano uliopo badala ya kuwa chanzo cha mfarakano na migogoro isiyokuwa na manufaa kati ya waumini, serikali na jamii kwa ujumla.