MAMA ALIYEMCHOMA MWANAE MIKONO NAE ASHUSHIWA RUNGU NA MAHAKAMA

0

 

Mahakama ya Wilaya ya Geita imemhukumu mkazi wa Kijiji cha Shahende, Mpipi Emanuel (33), kutumikia kifungo cha miaka mitano  jela kwa kosa la kumchoma moto mikono mtoto wake mwenye umri wa miaka 14.

Kitendo hicho kimemsababishia mtoto huyo maumivu makali na kushindwa kufanya mtihani wa taifa wa darasa la saba.

Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Samweli Maweda, baada ya mshtakiwa kukiri kosa lake hilo. Baada  ya mshtakiwa huyo kukiri kosa, Maweda alimwambia Wakili wa Serikali Shukran Msuya, amsomee mshtakiwa maelezo ya kosa.

Akisoma maelezo ya kosa, Wakili Msuya alidai kuwa Oktoba 4, mwaka huu, katika Kijiji cha Shahende, wilaya na mkoa wa Geita, mshtakiwa alimchoma moto mtoto wake (jina linahifadhiwa) kwenye mikono na kumpiga fimbo kwenye miguu na kumsababishia maumivu makali mwilini mwake.


Msuya alidai kuwa Oktoba 4, mwaka huu, katika kijiji cha Shahende, mshtakiwa alimchoma moto mtoto wake kwa madai kuwa alimwibia Sh. 30,000 na pia alimwibia bibi yake Sh. 1,000 ndipo akapata hasira na kumpiga kisha kumchoma moto kwenye mikono.

Alidai kuwa baada ya tukio hilo, mtoto alipelekwa katika Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Geita na kupewa fomu ya matibabu (PF30 na hatimaye kupelekwa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Geita kwa ajili ya matibabu.

Mwanasheria huyo alidai kuwa mshtakiwa alikamatwa na kufikishwa katika kituo cha polisi Geita na baada ya mahojiano alifikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.

Baada ya Wakili wa Serikali kumaliza kumsomea mshtakiwa maelezo ya kosa, Hakimu Maweda alisema mahakama inamtia hatiani mshtakiwa kwa kukiri kosa mwenyewe bila ya kulazimishwa na mtu.

Kabla ya kusomewa hukumu, Hakimu Maweda alimtaka mshtakiwa ajitetee ili mahakama impunguzie adhabu.

Mshtakiwa huyo alijitetea kwamba anaomba mahakama impatie adhabu nyepesi kwa kuwa ana watoto watano wanamtegemea na hana makosa ya nyuma na kwamba hilo ni kosa lake la kwanza.

Upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili Msuya alidai kuwa hana kumbukumbu ya makosa ya nyuma ya mshtakiwa lakini akaomba mahakama itoe adhabu kali dhidi ya mshtakiwa ili iwe fundisho kwake na wanawake wengine wenye tabia za kikatili kama yake.

Hakimu Maweda alitupilia mbali utetezi huo na kusema mshtakiwa kitendo alichokifanya ni cha kikatili tena ni cha kinyama kwa kumchoma moto mtoto wake na kushindwa kwenda shuleni kufanya mtihani wa kumaliza darasa la saba.

Aidha, Maweda alisema kitendo alichokifanya mshtakiwa kinakatazwa na sheria za nchi pia kimefanya mtoto huyo kushindwa kutimiza ndoto zake, hivyo mshtakiwa anahukumiwa kifungo cha miaka mitano jela ili iwe fundisho kwako na kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

 

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top