Kijana mmoja anayefahamika kwa jina la Matson Sanga amedaiwa kutoa vitisho kwa baba yake mzazi John Sanga (81) pamoja na mama yake mlezi Mariam Sanga (62) wakazi wa Mtaa wa Power House mjini Njombe kwa shinikizo la kuwataka wagawane mali na mama yake mzazi ambaye walitengana na baba yake huyo miaka 45 iliyopita.
Kwa mujibu wa Mzee Sanga amesema kijana huyo alifungua kesi kwa jina la mama yake ili ijulikane mama yake huyo ndiye anayedai hata hivyo wao hawana tatizo juu ya maamuzi ya kugawana mali isipokuwa kikwazo kilichopo ni vitisho vya kijana huyo ndivyo vinawakosesha amani pamoja na idadi ya mali alizo orodhesha ambazo nyingine ni mali walizochuma na mkewe wa sasa ambaye wameishi naye kwa takribani miaka 33.
Kutokana na Kuhofia Usalama wao Wazee hawa wakalazimika kukutana na mawakili wa kituo cha sheria na haki za binadamu ili kupata ushauri juu ya mkasa walionao.
Aidha akizungumza kwa njia ya simu kijana huyo amekana kuhusika na mgogoro huo huku akidai mama na baba yake ndiyo wenye mgogoro.