Kulingana na chifu wa kata ya Kiarukungu, Henry Kariuki, tineja huyo alikataa kumpa baba yake chakula kwa sababu mama yake Magdalene Wanja hakuwepo.
Marehemu Justus Mutiso alifika nyumbani mwendo wa saa 10:30 usiku na kuanza kumuitisha bintiye chakula ambaye alikataa kumpa.
Kwa mujibu wa ripoti ya polisi, msichana huyo aliamua kwenda kumchukua mama yake, ambaye alikuwa kwenye kanisa lililo umbali wa mita 500 kutoka nyumbani kwao.
"Ilinibidi niachane na maombi ya nilipopokea habari kwamba alihitaji kuandaliwa chakula cha jioni. Nilikimbia kurudi nyumbani na kutekeleza wajibu wangu kama mke lakini cha kusikitisha kilichofuata kilinifanya nishtuke vile vile,” mama huyo alisema.
Huku baba yake msichana huyo akiwa bado anashangazwa na tabia ya bintiye kumnyima chakula, aliamua kumwadhibu lakini mshukiwa alimdunga kisu.
Mwanamume huyo alikimbizwa hospitalini na alifariki alipokuwa akipokea matibabu katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Kibimbi. Kufutia tukio hilo, jamaa wametoa maoni kinzani huku bibi yake Veronicah Wanja, akifichua kuwa sio mara ya kwanza kwa mwanamume huyo ‘kumshambulia’ bintiye.
Nancy Kanini, dada yake marehemu hata hivyo, alisema kwamba msichana huyo alipaswa kumheshimu babake ili kuepuka majibizano yaliyosababisha kifo chake. "Mshukiwa alimuua kaka yangu na lazima aadhibiwe kulingana na sheria," alisema. Kulingana na chifu, waliweza kupata kisu ambacho msichana huyo alitumia kumuua babake.
Msichana huyo anazuiliwa katika Kituo cha Polisi cha Wang'uru na atafikishwa katika Mahakama ya Wang’uru leo Jumanne, Oktoba 25, baada ya uchunguzi kufanywa.
Chanzo: TUKO.co.ke