Mbunge wa jimbo la Makete mkoani Njombe Festo Sanga amelizungumzia sakata la matumizi ya stendi mpya Tandala iliyotakiwa kuanza kufanya kazi kuanzia Oktoba 1, 2022 kama ilivyotangazwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Makete ambapo mpaka sasa bado utaratibu huo uliotangazwa hauzingatiwi
Katika tangazo lililotolewa na kusainiwa na mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Makete William Makufwe ilisema mabasi yote yanayofika Tandala na Ikonda kutokea Mbeya na Njombe yatatakiwa kushusha abiria katika stendi mpya Tandala ambapo utaratibu huo ulitekelezwa kwa siku moja kabla ya kusitishwa
![]() |
Mh Mbunge jimbo la Makete akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ikonda |
Akiwa kwenye mkutano wa kuzungumza na wananchi Oktoba 10, 2022 kuhusu masuala mbalimbali ya maendeleo pamoja na kusikiliza kero zao katika kijiji cha Ikonda kwenye ziara yake ya kijiji kwa kijiji, Mbunge Sanga amesema suala hilo kwa sasa limetulia baada ya kushirikiana na kuweka mambo sawa, kwa kuwa si hekima mgonjwa kushushwa stendi ya Tandala badala ya hospitali kwa kuwa wanafika wakiwa katika hali tofauti tofauti
“Juzi hapa kulitokea vurugu vurugu za stendi, lakini si mambo yanakwenda sawa saivi, isaitsi sikhutulie (saizi si kumetulia), tuliona si hekima mgonjwa afike aanze kushushwa mwingine yupo kwenye machela, mwingine yupo kwenye wheel chair (kiti mwendo), mwingine yupo katika hali mbaya lazima tuwasaidie tuonyeshe ukarimu wa wilaya ya Makete” amesema Mbunge
Amesema wanachokitaka ni lazima magari yaingie kwenye stendi hiyo ya Tandala ili yalipe ushuru yakitoka yaendelee na safari, hivyo kusema magari ya abiria yasifike hospitali ya Ikonda wameona hawakutenda haki na huo sio ukarimu wa wanamakete
Katika hatua nyingine Mbunge Sanga amelazimika kutolea ufafanuzi suala la asilimia za vijiji kurudishwa kama ilivyokuwa awali, baada ya mkazi wa kijiji hicho Shaibu Mahenge kudai kukosekana kwa asilimia za vijiji kijijini hapo kunasabisha washindwe kukamilisha kwa wakati miradi ya maendeleo wanayoiibua
Ndipo mbunge huyo akatoa elimu kwa wananchi hao kwamba kumekuwa na vijiji vyenye mapato kidogo na vingine vina mapato mengi hivyo kwa kutegemea asilimia za makusanyo kutasababisha maeneo mengine kushindwa kupata fedha zinazotosheleza miradi ya maendeleo hivyo wakaona wazikusanye pamoja na kuzirejesha kupitia miradi iliyoibuliwa
Mbunge amewataka viongozi wa kata ya Tandala kuhakikisha wanaibua miradi na kuipeleka halmashauri ili yeye kama mjumbe wa kamati ya fedha aone mradi kutoka kata ya Tandala hususan kijiji cha Ikonda ili wajadili na wapitishe kiasi cha fedha kiletwe kwenye mradi kijijini hapo, kwa kuwa kama mradi hauji watawapa fedha wengine wanaoibua miradi na kupeleka halmashauri
“Kijiji cha Kiguru mapato yao kwa mwezi ni shilingi elfu tatu, ukienda Ihanga mapato yao kwa mwezi ni shilingi elfu moja na mia tano kwa mwezi, ukienda Ujuni mapato yao kwa mwezi ni milioni tano, ukija Ikonda mapato yenu kwa mwezi mmoja hayazidi laki tatu, sasa tukasema huyu wa Ihanga mwenye elfu moja mia tano, hii elfu moja mia tano itafanya nini, lazima tuchanganye fedha zote kwenye mfuko mmoja, ishu hapa ni mtendaji, diwani, watumishi wa kata hii kuhakikisha wanaibua miradi na wanaipeleka halmashauri, mimi mjumbe wa kamati ya fedha ya halmashauri nione mradi kutoka kata ya Tandala nione mradi kutoka kijiji cha Ikonda, halafu tujadili hawa wenzetu hawajapata muda mrefu tuwape milioni 10 yao, sasa kama mradi hauji tutawapa wale wanaoleta miradi” amesema mbunge Sanga
chanzo;edmo blog.