Na Gift Mongi Moshi
Katika kuhakikisha kuwa wakazi wa jimbo la Moshi Vijijini mkoani Kilimanjaro wanapata huduma za kijamii kama ilivyoainishwa kwenye ilani ya uchaguzi ya CCM ,(2020-2025)mbunge wa jimbo hilo Prof Patrick Ndakidemi amtembelea kata ya Kibosho Magharibi ambapo amekagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Kibosho Umbwe eneo la kwa Edita inayoendelea kujengwa kwa kiwango cha lami.
Mradi huo wa barabara wenye urefu wa mita 425 unatekelezwa na mkandarasi Kifuko Keko Furniture ambapo Mpaka Sasa umefika asilimia 95 hadi kukamilika kwake.
Benedict Charles ni mhandisi na msimamizi wa barabara hiyo ambapo amesema kuwa mradi huo ulipaswa uwe umekamilika mapema ila changamoto ya mvua imefanya kusimama kwa muda na kuwa sasa hivi wako mbioni kukamilisha.
Mhandisi Benedict amemweleza Prof Ndakidemi kuwa kwa sasa wako katika hatua ya kuweka mitaro na baada ya wiki tatu kuanzia hivi sasa watakuwa wamemalizia kazi ya kuweka lami.
Hata hivyo Prof Ndakidemi ameeleza kufurahishwa na jinsi kazi hiyo inavyokwenda na amemsihi mkandarasi amalize mapema ili wananchi waweze kutumia barabara kama ilivyopangwa kwani sehemu iliyobaki imekuwa ni kero kwa wananchi wa Kibosho Magharibi.
Naye Peter Mushi mkazi wa eneo hilo amesema kukamilika kwa barabara hiyo kutaenda kuondoa kero ya usafiri iliyodu.u kwa kipindi kirefu lakini pia kutaenda kuchochea kukua kwa maendeleo katika eneo hilo.
Doreen Olomi amesema kukamilika kwa barabara hiyo kutaenda kurahisisha usafirishaji hususan kwa upande wa wanawake kwani wengi wao ni wajasiriamali hivyo gharama za usafirishaji zitaenda kupungua.