POLISI WATAKA SOMO LA UKATILI LIANZISHWE SHULENI KUWALINDA WATOTO

0

 Katika kukabiliana na matukio ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto wilayani Ikungi mkoani Singida, uongozi wa Jeshi la Polisi umesema unachukua hatua kali dhidi ya watuhumiwa ambapo watu wawili wamehukumiwa vifungo miaka 30 jela na mmoja kifungo cha maisha ndani ya kipindi cha miezi miwili.

Mkuu wa Polisi Wilaya ya Ikungi, Suzana Kidiku alibainisha hayo jana wakati Shirika la Empower Society Transform Lives (ESTL) linalojihusisha na masuala ya kupinga ukatili wa kijinsia, lilipozindua rasmi huduma za elimu na uwezeshaji jamii kwenye wilaya hiyo.

Alisema Jeshi la Polisi limekuwa kwenye harakati mbalimbali za kukabiliana na matukio ya ukatili wa kijinsia kwa nyakati tofauti ambapo katika kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba mwaka huu limefanikiwa kunusuru kwa kuwarejesha shuleni wanafunzi watatu ambao walikuwa hatarini kukatisha masomo yao kutokana na matukio ya ukatili.

Kidiku alisema jeshi hilo katika kipindi hicho limefanikiwa kufikisha kesi tatu za matukio ya ukatili wa kijinsia kwenye vyombo vya sheria ambapo mahakama iliwakuta watuhumiwa na hatia na wawili walihukumiwa vifungo vya hadi miaka 30 huku mmoja akiadhibiwa kifungo cha maisha.

Mkaguzi wa Uhamiaji Wilaya ya Ikungi, Abel Shindayi alisema kuna haja mamlaka za elimu kufanya marekebisho ya mfumo wa mtaala wa elimu uliopo kwa kuongeza kipengele cha somo la ukatili wa kijinsia ili wanafunzi wafundishwe na kuwa na uelewa mpana wa masuala hayo.

Mkurugenzi wa ESTL, Joshua Lisu alisema Wilaya ya Ikungi  ina vihatarishi vikubwa vya matukio ya ukatili kwa wanawake na watoto kutokana na jiografia yake ya mipaka na wilaya za jamii ya wafugaji za Hanang (Manyara) na Kondoa (Dodoma) ambazo zimegubikwa na matukio ya ukeketaji.

Alisema shirika hilo lisilo la kiserikali kwa udhamini wa Ubalozi wa Finland, Uholanzi na Shirika la Foundation Civil Society (FCS) katika kipindi cha miaka minne (2018-2022 limefanikiwa kuzifikia takribani kata 28 ndani ya Wilaya za Singida Manispaa na Singida Vijijini kwa utekelezaji wa huduma kama hizo.

Huduma nyingine walizofanikiwa kuzitoa kwenye maeneo hayo ni pamoja na uanzishwaji wa utaratibu wa utoaji huduma mbalimbali ndani ya eneo moja (One Stop Centre), uundaji wa kamati za MTAKUWWA zipatazo 39 sambamba na uanzishaji wa mfumo maalum wa TEHAMA ambao umekuwa ukifanya kazi ya kufuatilia kesi za matukio ya ukatili.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

 

 

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top