Bibi kikongwe mmoja (75) mkazi wa mtaa wa Bong’ola Manispaa ya Morogoro aliyefahamika kwa jina la Mwajuma Sadru, amekutwa akiwa amefariki dunia na mwili wake kutelekezwa kisha kufunikwa kwa mawe umbali wa mita 180 kutoka nyumbani kwake eneo la kwa masikini.
Akizungumza na Michuzi Tv mtoto wa marehemu John Dofriana amesema kuwa alipata taarifa za kutoonekana kwa mama yao akiwa jijini Dar es Salaam jambo lililopelekea kusafiri hadi mkoani Morgoro na kuanza kumtafuta ndipo walikuta mwili wake ukiwa umetelekezwa ukiwa umefunikwa na mawe.
Aidha John alisema kuwa mama yake alikuwa akiishi kwa miaka mingi katika mtaa huo na alikuwa akiishi na dada wa kazi huku akihudumiwa kwa karibu na mwanaye mkubwa hadi tukio hilo la kikatili lilipo mkuta.
“Kimsingi tukio limetokea jana usiku na kaka aliporudi nyumbani kutoka kwenye majukumu yake alikuta tukio limeshatokea na alijaribu kupigia simu lakini haikuwa haipokelewi na wakati akiendelea kumtafuta ndipo waliipata simu ikiwa na damu nyingi ndipo wakagundua kuwa mama anashida na mimi nikaaza safari usiku huohuo kuja hapa Morogoro.” Alisema John mtoto wa marehemu.
Tatu Juma ni jirani wa marehemu ambaye alisema kuwa bibi huyo anayefahamika kwa jina la mtaani kama bibi mzungu alikuwa mcheshi nan a alikuwa akiongea vizuri na watu na kwamba siku ya tukio walipata tarifa kisha kufika nyumbani kwake ndipo walianza kumtafuta bila mafanikio hadi ulipopatikana mwili wake ukiwa umefunikwa kwa mawe eneo la kwa masikini jirani na nyumbani kwa marehemu.
“Bibi Mzungu ni jirani yangu amehamia hapa kwa muda mrefu sana na alikuwa hana tatizo na mtu ni mcheshi na sijawahi kusikia amegombana na mtu hapa mtaani lakini hili tukio lililotokea limenisikitisha sana.” Alisema Tatu jirani wa marehemu.
Kwa upande wake mwenyekiti wa tawi Shabani Juma alisema tukio hilo limetia doa mtaa na kwamba ameliomba jeshi la polisi Mkoa wa Morogoro kuwachukuliwa hatua wale wote wanaojichukulia sheria mkononi.
Akizungumza na waandishi wa Habari Kamanda wa polisi MKoa wa Morogoro ACP Fortunatus Msulimu alithibitisha kutoka Kwa tukio Hilo ambapo alisema chanzo Cha kifo Cha Bi. Mwajuma ni alipigwa na kitu kizito kichwani.
Alisema kufuatia tukio hilo jeshi la Polisi linamshikilia bwana Nestory Elias( 62) Mkazi wa Bon'gola Kata ya Kilakala kwaajili ya uchunguzi wa awali na kwamba inaelezwa kuwa marehemu alikuwa na mgogoro wa Ardhi na mtuhumiwa huyo.
Tukio hilo limetokea October 3, 2022 majira ya saa12 Asubhi katika mtaa wa Bong’ola Kata ya Kilakala Manispaa ya Morogoro ambapo jeshi la polisi limefika katika eneo la tukio na kuchukua mwili wa marehemu kwa ajili ya uchunguzi zaidi.