Wakazi wa Kijiji cha Nyamakobiti, Kata ya Majimoto, mkoani Mara, wametaka warejeshewe madaraka ya kutumia mila na desturi zao katika kushughulikia wahalifu sugu, wakiwamo majambazi, ikiwa polisi watatishwa na maneno ya wanasiasa.
Hayo yameelezwa kupitia mkutano wa hadhara, ulioandaliwa na uongozi wa kijiji hicho, ili wajadili hali ya ulinzi na usalama wao, ikiwa ni wiki moja tangu watu watatu walioshukiwa kuwa majambazi, wauawe kwa risasi katika operesheni maalumu iliyofanywa na Polisi Mikoa ya Mara, Simiyu, Mwanza na Kanda maalumu ya Tarime/Rorya.
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kitarahota B, Chacha Charles alisema licha ya tukio hilo, ujambazi bado ni changamoto kwao, wanahitaji operesheni za ulinzi ziendelee.
Leonad Renkerenge, alisema badala ya kumhangaisha Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Camillius Wambura, waruhusiwe kutumia mila na desturi kama ilivyokuwa zamani, kushughulikia majambazi, ambao wanawafahamu kwa sababu wanaishi nao.
Bhoke Karogo (68) ambaye ni mlemavu wa macho, alisema Septemba 27 mwaka huu usiku, mlango wa nyumba yake ulivunjwa na wahusika walimuibia kuku 20, ambao aliwafuga kwa kipindi kirefu.
“Ilikuwa nikipata shida nauza kuku, najihudumia sasa wamewaiba wote,” alisema akishindwa kuzuia machozi.