Na.OR-TAMISEMI
Jumla ya watahiniwa 1,384,340 wameanza mitihani yao ya kumaliza elimu ya msingi nchini huku idadi ya watahiniwa kwa mwaka 2022 ikiongezeka ukilingalinisha na mwaka 2021 ambapo jumla ya watahiniwa walikuwa 1,132,084 sawa na ongezeko la watahiniwa 252,256 katika mwaka huu.
Hayo yamebainishwa Septemba 5,2022 na Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Elimu Dr. Charles Msonde na kuongeza kuwa katika idadi hiyo wavulana 661,276 na 723, 064 wasichana wanaendelea na mitihani yao ambayo itadumu kwa siku mbili kuanzia Septemba 5 hadi 6, 2022.
Msonde amesema Serikali imejipanga vizuri kusimamia mitihani hiyo kupitia viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa na ameendelea kutoa wito kwa viongozi hao kufuata kanuni na taratibu za usimamizi wakati wote wa mitihani.
"Nimepita shule kadhaa katika Mkoa wa Dar es Salaam hali ni nzuri wanafunzi wameanza kufanya mitihani yao vizuri kwa utulivu na watendaji wamejipanga kusimamia vizuri kama tulivoelekeza niendelee kusisitiza mitihani hii ifanyike kwa kuzingaitia kanuni na taratibu” Msonde
Aidha Msonde amewataka wanafunzi wote ambao wanaendelea na mitihani hiyo kutokuwa na wasiwasi kwakuwa mitihani hiyo inatungwa ndani ya mada walizofundishwa katika masomo yao, amewasisitiza kufanya mitihani hiyo kwa umakini na umahiri ili waweze kuendelea na masomo ya elimu ya Sekondari.
Mtihani wa kumaliza Elimu ya Msingi kwa mwaka huu unafanywa katika masomo sita ambayo ni Sayansi na Teknologia, Hisabati, Lugha ya Kingereza, Maarifa ya Jamii na Stadi za Kazi, Uraia na Maadili pamoja na Kiswahili.
Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) inatoa salamu za kheri kwa watahiniwa wote ambao wameanza mitihani yao ya kumaliza elimu ya Msingi.