Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora imewabadilishia mashitaka ya mauaji washitakiwa wawili na kuwahukumu kifungo cha nje cha mwaka mmoja baada ya kuwakuta na hatia ya kuua bila kukusudia.
Uamuzi huo umefikiwa Oktoba 13 na hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mkoa wa Tabora, aliyekasimishwa Mamlaka ya ziada, Jovin Katto baada ya kusikiliza maelezo ya upande wa mashitaka na utetezi.
Katika kesi hiyo, washitakiwa Mrisho Ramadhani na mwanaye Ramadhani Mrisho ambao ni wakazi wa Manispaa ya Tabora, walidaiwa kumshambulia Hussein Ibrahimu na kumsababishia majeraha Aprili 14, 2020 na alifariki kesho yake baada ya kufikishwa hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Tabora, Kitete.
Akichambua maelezo ya mashahidi wa kesi hiyo, Hakimu Katto, amesema kuwa Mahakama imejiridhisha kwamba Hussein Ibrahim ambaye kwa sasa ni marehemu ndiye aliyejisabababishia kifo chake kutokana na kuanzisha vurugu na kuwatolea matusi washitakiwa.
Akisoma hukumu hiyo, hakimu Katto, amesema kuwa Mahakama haina haja ya kujaza Magereza na kwa kuzingatia utetezi wao kwamba miaka miwili waliyokaa mahabusu imekuwa funzo kwao watatumikia kifungo cha miezi 12 cha nje.
Hakimu Katto amesema kwa kutumia mamlaka aliyopewa na kwa kutumia kifungu namba 300(1), anabadilisha shitaka la mauaji na kuwa kosa dogo la kuua bila kukusudia.
Kifungu hicho cha sheria ya makosa ya jinai kinaeleza kuwa, wakati mtu anashtakiwa na kosa na maelezo yanathibitisha kwa kupunguza kosa na kuwa kosa dogo, anaweza kutiwa hatiani kwa kosa hilo dogo japokuwa hakushtakiwa na kosa hilo.