Ndege ya Shirika la ndege la Air Tanzania (ATCL) imeshindwa kutua katika uwanja wa ndege wa Bukoba Mkoani Kagera kutokana na hali mbaya ya hewa.
Baadala yake ndege hiyo imelazimika kutua salama
katika uwanja wa ndege Jijini Mwanza.
Alipoulizwa kwa njia ya simu Novemba 17, 2022
kuhusu tukio hilo, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri wa anga Tanzania (TCAA) Hamza Jabir
amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.
“Ni kweli nimepata taarifa ndege ya Air Tanzania imeshindwa kutua kutokana na hali mbaya ya hewa, kulikuwa na ukungu, mvua, radi na giza uwanja ukawa hauonekani, kwa hiyo rubani akafuta safari na kurudi Mwanza na ametua salama” Mkuugenzi TCAA
Kushindwa kutua kwa Air Tanzania katika uwanja huo ni siku kumi tu tangu kutokea kwa ajali ya ndege ya Shirika la ndege la Precision Air, ambayo ilikuwa inatokea Dar-es-Salaam kwenda Bukoba kushindwa kutua katika uwanja wa Bukoba kutokana na hali mbaya ya hewa na kisha ndege hiyo kuanguka katika ziwa Victoria na kupelekea vifo vya watu 19 na majeruhi 24.
Ajali ya Shirika la ndege la Precision Air ilitokea November 7, 2022 saa 2 asubuhi.