Mwanamume mmoja mkazi wa kaunti ya Mombasa huko Kenya alikamatwa na maafisa wa polisi baada ya kumdunga kisu mkewe kutokana na hatua yake ya kulala kwenye sofa badala ya kitanda chao cha ndoa.
Mshukiwa anaripotiwa kumdunga mwenzi huyo wake mara kadhaa mbele ya watoto wao ambao waliwajulisha watu kuhusu ugomvi wa wazazi wao.
Inaripotiwa kuwa mzozo ulianza sebuleni ambapo mwanamume huyo alijaribu kumburuta mkewe kwenye chumba cha malazi na alipodinda, mvutano mkubwa ukazuka na kupelekea kifo cha mwanamke huyo.
Tukio hili la mkewe lilizua hisia, sio miongoni mwa wanakijiji pekee mbali pia kwa kamanda wa polisi Stephene Matu ambaye alilaani vikali tabia hiyo ya kinyama. Aliongeza kuwa mshukiwa anazuiliwa katika kituo cha polisi huku uchunguzi zaidi ukiendelea ili kubaini kiundani kilichotokea na sheria kuchukua mkondo wake.
"Alikamatwa kufuatia tukio hilo. Anashughulikiwa ili afikishwe mahakamani kuhusiana na mauaji hayo, hivyo uchunguzi unaendelea ili kupata ushahidi wa kutosha na kubaini nini halisi kilitokea," alisema.
Matu pia aliwasihi wanandoa kutafuta suluhu bora ya kuzima migogoro baina yao wala sio kukatiza maisha ya wenzao.
Alisema, ''Tunawahimiza wanandoa kutatua maswala ya wanandoa kwa njia ya amani wala sio kujawa na hasira nyingi inayopelekea kukatiza maisha ya mtu."