Mtemi wa Jeshi la Jadi Sungusungu kijiji cha Lunguya, Julius Kahenyela Manyama
Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) umeendesha Mkutano wa Tathmini ya kazi zilizofanywa na Kituo cha Taarifa na Maarifa kata ya Lunguya na wanajamii kuanzia mwaka 2020 hadi 2022 kuhusu ukatili wa kijinsia ambapo miongoni mwa mijadala iliyotawala ni pamoja kuwepo kwa Biashara haramu ya Ngono maarufu ‘Mchemsho’ kwenye migodi ya Nyamishiga, Kalole na Nyangalata inayofanywa na watoto wadogo na watu wazima.
Mkutano huo umefanyika Jumatano Novemba 16,2022 na kukutanisha makundi mbalimbali ya kijamii wakiwemo watu maarufu, waganga wa jadi,Wakango, viongozi wa dini, mila, serikali, sungusungu, vijana, wanafunzi na kituo cha taarifa na maarifa Lunguya.
Mwezeshaji kutoka Mtandao wa Jinsia (TGNP) Aluwa Hamisi Mkilindi amesema Lengo la Mkutano huo ni kujadili hali halisi ya ukatili wa kijinsia kabla na baada ya kuanzishwa kwa Kituo cha Taarifa na Maarifa Lunguya mwaka 2020 na Namna kituo cha taarifa na maarifa kinavyoshirikiana na jamii na serikali katika kutokomeza matukio ya ukatili wa kijinsia.
Diwani wa kata ya Lunguya Benedicto Manuari amesema hali ya sasa tofauti ni kubwa sana ambapo masuala ya mimba za wanafunzi yamepungua, utoro umepungua na ukatili umepungua.
“Pamoja na uwepo wa migodi lakini vijana wetu wanajitambua wameshajua wafanye nini, tofauti na mwanzo ambapo walikuwa wanajua ni kuolewa tu, hawakujua madhara ya mimba za utotoni kwa kweli mabadiliko ni makubwa, watoto wameshajitambua”,amesema Manuari.
Wanafunzi walioshiriki mkutano huo wamesema awali walikuwa wanaachishwa shule, wanafunzi walikuwa wanatoka umbali mrefu kwenda shule, watoto wa kike hawakupewa nafasi ya kwenda shule na wengine walikuwa wanabakwa lakini sasa hali imebadilika mambo yanaenda vizuri.
Mwenyekiti kituo cha taarifa na maarifa kata ya Lunguya, Loyce Kabanza amesema tofauti na hapo awali hivi sasa Wanawake wanashiriki kwenye machimbo kama wanaume, wakango wamepunguza matusi na wanaendelea kutoa elimu kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia.
Licha ya mafanikio makubwa yaliyofikiwa ikiwemo kupungua kwa mimba na ndoa za utotoni, utoro shuleni, wanawake kunyanyaswa lakini suala la Biashara ya ngono kwenye maeneo ya migodi inayofanyika kati ya wasichana wadogo na wanaume watu wazima lakini pia akina mama watu wazima na wavulana wadogo kwa gharama ya shilingi 3,000/= imetajwa kuwa changamoto kubwa inayosababisha mmomonyoko wa maadili na kuchochea ukatili wa kijinsia.
Mmoja wa Washiriki wa mkutano huo Bi. Mariam Paul Kadushi ambaye ni mwanakituo cha Taarifa na maarifa Lunguya ameeleza kusikitishwa na biashara ya ngono inayoendelea kwenye migodi ya dhahabu iliyopo katika kata ya Lunguya ambapo mabinti wadogo wamekuwa wakiuza miili yao kwa wanaume wanaofanya kazi ya uchimbaji madini.
“Watoto wetu hawapo salama sasa kwenye migodi, mabinti wadogo wanafanya ngono na wababa watu wazima lakini pia vijana wetu wa kiume nao wanafanya ngono na akina mama watu wazima, haya mambo ya hovyo kabisa, naomba Jeshi la Jadi Sungusunguna serikali muingilie kati suala hili, akina baba wanachukua mali za familia na kwenda kuuza wapate pesa ya MCHEMSHO (kufanya ngono)”,amesema Bi. Mariam.
JE! UNAJUA UNAWEZA KUTENGENEZA KIPATO CHA ZAIDI YA $150 KUPITIA MTANDAONI?