Wanamtandao wa kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia Kisiwani Pemba, wameombwa kuzidisha juhudi ya kutoa elimu kwa wananchi katika kupambana na vitendo vya udhalilishaji ambavyo vinavyookena kukithiri kila uchao.
Mapema akizungumza na wanamtandao Kisiwani Pemba, katika mkutano wa kujadili ripoti ya mwaka ya ufuatiliaji wa vitendo vya udhalilishaji, afisa mradi wa kupinga vitendo vya udhalilishaji kutoka chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania Tamwa, Zanzibar Zaina Salum Abdalla, amesema wanamtandao hao wanakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo kukosa mashirikiano kutoka kwa baadhi ya wananchi wakati wanapokuwa katika utekelezaji wa majukumu yao, jambo ambalo hupelekea kuzorota kwa kesi za udhalilishaji.
Ameongeza kuwa katika mikutano waliyoifanya katika kisiwa cha Unguja wananchi wengi wamekuwa wakivitupia lawama baadhi ya taasisi za Serikali ikiwemo Jeshi la Polisi, Ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka pamoja na mahakama jambo ambalo linawarudisha nyuma wananchi hao katika kupambana na vitendo hivyo.
Kwa upande wake, Afisa ufuatiliaji na tathmini kutoka Tamwa Zanzibar Mohammed Khatib Mohammed, amesema kuripotiwa kwa matukio ya vitendo vya udhalilishaji katika vyombo mbali mbali vya habari inasaidia kwa kiasi kikubwa Serikali pamoja na jamii kuona ukubwa wa jambo hilo na kuandaa mipango madhubuti katika kukabiliana janga hilo.
Nae, Mratibu wa Tamwa Kisiwani Pemba Fat-hiya Mussa Said, amesema wakati umefika kwa jamii kuzingatia mila na desturi katika malezi ya watoto ili vijana waweze kufahamu mabadiliko yao ya kimwili sambamba na afya ya uzazi.
Akisoma ripoti kwa niaba ya wanamtandao wa kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia Wilaya ya Mkoani, Shaaban Juma Kassim, a mesema kutoka mwezi January hadi November 2022, jumla ya kesi 26 za udhalilishaji zimeripotiwa, ambapo kesi za kubaka ni 19, kutorosha 1, kulawiti 4, Utelekezaji 1, kujaribu kulawiti na kukashifu 1.
Aidha amesema, kesi sita (6) kati ya kesi zote za kubaka zimesalia Katika vituo vya Polisi, kesi nne (4) zinaendelea mahakamani, kesi moja (1) imehukumumiwa na mshitakiwa amekutwa na hatia na kuhukumiwa kutumikia chuo Cha mafunzo, zilizoondolewa mahakamani ni kesi nne (4) na iliyofanyiwa suluhu ni kesi Moja (1) ya Jambangome na watuhumiwa waliotoroka ni tatu (3).
Kwa upande wa wanamtandao wa Wilaya ya Wete wakiwakilishwa na Rashid Hassan Mshamata, wamesema kutoka mwezi January hadi November 2022, jumla ya kesi mpya 62 za ukatili wa kijinsia zimeripotiwa, ambapo kesi za kubaka ni 30, kutorosha 9, shambulio la aibu 6, kunajisi mvulana 8, kuingilia kinyume na maumbile 1, Ujauzito 3, Utekelezaji 1, kulawiti 2, udhalilishaji wa kielimu 1 na Udhalilishaji mkubwa 1.
Nao baadhi ya wanamtandao hao wamesema miongoni mwa changamoto zinazowakabili katika kukabiliana na vitendo hivyo vya udhalilishaji ni pamoja na wanafamilia kutokutoa ushirikiano pindi zinapotokea kesi hizo.
"Kwakweli kuna sababu nyingi mno zinazopelekea kesi za udhalilishaji kushindwa kumaliza katika Jamii zetu na moja miongoni mwa sababu hizo Jamii kutokuwa tayari katika kutokomeza vitendo hivyo, Kwa mfano sisi wanamtandao tunajitoa kwa hali na mali tunaposikia tu taarifa za vitendo hivyo lakini chakusikitisba unakuta familia zenyewe zinashirikiana na kuanza kusuluhishana kienyeji na kama titashikilia kuipelekea kesi mahakamani basi mashahidi hawaji Mahakamani kutoa ushahidi" Bakar Khamis Khalid, msaidizi wa sheria Wilaya ya Wete
Ripoti hiyo ya mwaka kuhusu ufuatiliaji wa vitendo vya ukatili wa kijinsia Kisiwani Pemba, imeonesha kuwepo kwa changamoto kadhaa katika kesi za udhalilishaji ikiwemo baadhi ya wahanga wanawake wenye umri kati ya miaka 16 na 17 kukataa kutoa ushahidi mahakamani.