WANAHARAKATI WA KUPAMBANA NA VITENDO VYA UKATILI WA KIJINSIA PEMBA, WAZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI, KUELEKEA SIKU 16 ZA KUPINGA UKATILI KWA WANAWAKE NA WATOTO WA KIKE DUNIANI.

Hassan Msellem
0

Wanaharakati wa kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia Pemba, wameiomba Serikali kuimarisha mifumo yake ya takwimu za matukio ya ukatili wa kijinsia ili kutoa mwenendo halisi wa matukio hayo.

Ombi hilo limetolewa na mwenyekiti wa kamati za asasi za kiraia Pemba Ndugu Nassor Bilal Ali, amesema kuimarika kwa mifumo ya takwimu kutaweza kuonesha hali halisi wa mwenendo wa kesi hizo ikiwemo kesi zinazoendelea mahakamani na ambazo zimeshatolewa uwamuzi.

 

Mwenyekiti huyo ameshauri kuwepo kwa mpango wa maalum wa kuwatambua na kuwathamini wanaharakati na mahakimu wanaofanya vizuri katika usikilizaji wa kesi hizo sambamba na kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote wanaohusika katika ucheleweshaji wa kesi hizo.

 

Ameongeza kuwa kwa mujibu wa ripoti ya takwimu za ukatili na udhalilishaji wa kijinsia Zanzibar kutoka ofisi ya mtakwimu mkuu wa Serikali Zanzibar kwa mwezi Agosti 2022, jumla ya kesi 131 za ukatili na udhalilishaji wa kijinsia yameripotiwa ambapo waathirika wanawake ni 12 sawa na asilimia 9.2 na watoto ni 119 sawa na asilimia 90.8 miongoni mwao wasichana walikuwa 84 sawa asilimia 70.6 na wavulana 35 sawa na asilimia 29.4.

Mwenyekiti wa kamati za asasi za kiraia Pemba Ndugu Nassor Bilal Ali akisoma ripoti.

Akijibu maswali yaliyoulizwa na waandishi waliohudhuria katika mkutano huo Mratibu wa Tamwa Pemba, Fat-hiya Mussa Said, amesema takwimu zinaonesha wananchi wengi wamepata uelewa juu ya kuripoti matukio ya udhalilishaji katika vyombo vya Sheria ikilinganishwa na hapo awali.


“Sitaki nitoe idadi halisi kwasababu hatuna mamlaka ya kutoa idadi ya kesi zilizotokea lakini kwa tathmini za haraka haraka zinaonesha kuwa wananchi wengi wamekuwa na uelewa kuhusu kuripoti kesi za udhalilishaji pindi zinazapotokea na ndio maana kila siku munasikia kwenye vyombo vya habari kuhusu kesi mpya zinazoripotiwa na zile zinazotolewa hukumu jambo ambalo zamani haikuwa hivyo” Mratibu Tamwa, Pemba


Kuhusu umri wa msichana ukupunguziwa umri wa kutambuliwa kuwa mtu mzima kutoka miaka 18, amesema suala hilo ni haki msingi kwani licha ya hoja kuwa baadhi ya wasichana wenye umri wa miaka 15 hadi 17 kuchangia katika mazingira ya ubakaji na kutokutoa ushahidi mahakamani, kuna haja ya kutumika kwa njia mbadala za kuhakikisha wasichana wanajiepusha na vitendo hivyo pamoja kupewa adhabu stahiki endapo atakataa kutoa ushahidi mahakamani pindi akifanyiwa vitendo vya udhalilishaji.


“Suala la kupunguzwa kwa umri wa utu uzima kwa wasichana suala hili ni suala la kimjadala na ifike wakati kama wanaharakati tunapodai kuwa mtoto wa kike apunguzwe umri katika makosa haya mi nadhani hatutowatendea haki watoto wakike na tutaendelea kuwadhalilisha lakini wapo wanawake wenye umri wa miaka 35 hadi 40 nao wanabakwa je, nao tuseme hawajabakwa au wamesababisha wenye mazingira ya kubakwa? Sasa mimi niwaombe tu kwamba tuendelee kutafuta moarobaini wa hawa watoto wanafanyiwa udhalilishaji lakini kwa kutokujielewa wanashindwa kuzisimamia zile kesi kwakuwapa sapoti wale ambao wamewadhalilisha” alisema


Akikazia majibu hayo, mratibu huyo amewaomba wanaharakati wa kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia kuongeza juhudi za kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kutambua haki na wajibu wao katika kupambana na kesi hizo kusudi kutokomeza janga hilo.

 

Tatu Abdalla Msellem, ni Mkurugenzi wa jumuiya Tumaini Jipya Pemba (TUJIPE) amesema katika kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia na udhalilishaji wanashirikiana na wadau mbali mbali ikiwemo viongozi wa dini ili kila mdau aweze kushiriki katika mapambano hayo.

Tatu Abdalla Msellem, ni Mkurugenzi wa jumuiya Tumaini Jipya Pemba (TUJIPE).

Hafidh Abdi Said, ni Mkurugenzi wa jumuiya ya Kupunguza Umaskini na Kuboresha Hali za Wananchi (KUKHAWA), amesema kutokana na uzito wa janga la ukatili wa kijinsia na udhalilishaji jumuiya hiyo imechukua jitihada za kuhakikisha wanatoa elimu kwa kamati ambazo zinajukumu la kutoa elimu ya vitendo hivyo katika jamii.

Hafidh Abdi Said, ni Mkurugenzi wa jumuiya ya Kupunguza Umaskini na Kuboresha Hali za Wananchi (KUKHAWA).

Mkutano huo uliyowajumisha wanaharakati wa asasi za kiraia pamoja waandishi wa habari kisiwaani Pemba ni uzinduzi wa kuelekea katika kilele cha siku 16 za kupinga vitendo vya ukatili wa wanawake na watoto wa kike duniani, ambapo kaulimbiu ya kimaitaifa ya mwaka huu 2022 inasema “KUUNGANISHA UANAHARAKATI KUTOKOMEZA UKATILI DHIDI YA WANWAKE NA WASICHANA”.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

 

 

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top