Wananchi wa kijiji cha
Ivalalila mamlaka ya mji mdogo wa Iwawa wilayani Makete Mkoani Njombe wamesema
kuwa kwa sasa kipigo katika ndoa kimekuwa pande zote mbili bila kujali jinsia.
Wakizungumza katika
mkutano wa hadhara katika kijiji hicho uliolenga kujengeana uelewa juu ya
masuala ya ukatili kupitia mradi wa Mwanamke Imara chini ya WLDAF,wamesema kuwa
baada ya kuendelea kutangazwa usawa wa kijinsia kumechangia wanawake kuwapiga
wanaume.
Wanaume wanaaakili na wanawake
wanaakili,unaweza ukajipanga leo umempiga si ndio,siku nyingine unajisahau
anasema zamu yako leo unapigwa mwanaume’ amesema mmoja ya wanaume.
Baadhi ya wanawake
katika mkutano huo wamesema kuwa wanaume wengi wamekuwa wakishindwa kutekeleza
majukumu yao ikiwemo kuwajibika kutoa matunzo.
‘Unakuta mwanaume
anachelewa kurudi nyumbani,anafika anataka chakula anakuuliza mbona hakuna
nyama anataka wewe mwanamke ukatafute mboga nzuri’Amesema mmoja ya mwanamke.
Mwezeshaji Thomas Mponda kutoka Mradi wa Mwanamke
Imara amesema vitendo vya ukatili havikubaliki na kuwataka wanaume kwa wanawake
kuacha tabia ya kuwanyanyasa wenzao kulingana na jinsia zao.
‘Moja wapo ni
ubakaji,kulazimishwa kufanya ngono lakini inaenda mbali sana hata kumshikaa mtu
sehemu zake za siri bila ridhaa yake,hivyo vyote ni vitendo vya ukatili’
amesema Thomas
Kwa upande wake Wakili wa Mradi wa Mwanamke Imara
Bi. Suzan Kiwanga amesema kumekuwa na mtazamo katika jamii kuwa Dawati la
Jinsia ni kwa ajili ya wanawake na watoto pekee jambo ambalo sio sahihi na
kuwataka wanaume nao kutumia dawati la Jinsia kuripotiwa vitendo vya ukatili
wanapotendewa na wanawake.
Amesema Mwenendo wa
maisha ya kila siku ya wanafamilia ndio matokeo ya familia ijayo ya watoto wao
ikiwa baba atampiga mkewe basi mtoto hata yeye akiwa na familia ataona ni jambo
la kawaida.
Amoni Mapunda kutoka Ofisi ya Ustawi wa Jamii
Wilaya ya Makete amewasihi wananchi kuendelea kuwatumia maafisa Ustawi waliopo
kuanzia ngazi za Kata na viongozi wa vijiji kuripoti matukio ya ukatili ili
kuwepo na usawa wa kijinsia kwa watu wote.
Philipina Mkumbo Afisa upelelezi Wilaya ya Makete
akizungumza kwenye Mkutano huo amesema, matukio ya ukatili yameendelea
kuripotiwa katika Dawati la Jinsia Kituo cha Polisi Makete na vituo vidogo vya
Polisi lakini wanaendelea kutoa elimu na ushauri namna ya kukabiliana na
matukio hayo ya ukatili.
TAZAMA VIDEO HII ITAKUSAIDIA KUSAKA FURSA MTANDAONI