Watumishi watatu wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete mkoani Njombe wamefukuzwa kazi kutokana na utoro kazini, maamuzi ambayo yameridhiwa na baraza la madiwani la halmashauri hiyo
Uamuzi huo umefikiwa baada ya baraza la madiwani lililoketi leo Novemba 2, 2022 kujigeuza kama kamati kwa lengo la kujadili masuala ya kinidhamu ya watumishi ambapo wametoka na maamuzi hayo
Kaimu mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Makete Hawa Kader ametangaza maamuzi hayo katika kikao hicho na hatimaye baraza hilo kuridhia ambapo amesema baraza hilo halitakuwa tayari kufanya kazi na watumishi wazembe
Amewataja watumishi hao waliofukuzwa kazi kuwa ni Ones Ngogo aliyekuwa Afisa Mtendaji wa Kijiji aliyekuwa mtoro kwa siku 33, Sijali Mbwilo aliyekuwa Afisa Mtendaji wa kijiji aliyekuwa mtoro kwa siku 150 pamoja na Bakari Sembe aliyekuwa Afisa Kilimo kutokana na kuwa mtoro kwa muda wa siku 5
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Makete William Makufwe akizungumzia suala hilo amesema hakuna hasara yoyote serikali iliyoipata kutokana na utoro wa watumishi hao kwani walichukua hatua za kusimamisha mishahara yao tangu awali huku akiwataka watumishi kufanya kazi walizoomba
Amesema hatua zitaendelea kuchukuliwa kwa watumishi watoro kazini na kushangazwa na watumishi wanaochezea kazi ili hali mitaani kuna watu wengi ambao wanahitaji kuajiriwa.