WALIMU WENYE ULEMAVU WAZIDI KUIKUMBUSHA SERIKALI

0

Walimu wenye ulemavu Manispaa ya Moshi Mkoani Kilimanjaro wameiomba serikali kuendelea kuwapa kipaumbele na kuwaamini katika nafasi na majukumu mbalimbali ili waweze kuonesha uwezo wao.


Wametoa rai hiyo Novemba 9 mwaka huu wakati wa kikao maalumu kilicho wakutanisha pamoja na  Chama cha Walimu Manispaa ya Moshi kwa lengo la kufahamiana na kueleza changamoto zao katika maeneo yao ya kazi ili ziweze kufanyiwa kazi na kuwa katika mazingira rafiki muda wote wanapo timiza majukumu yao.


Walimu hao wameeleza kuwa bado zipo changamoto zinazo wakabili katika maneo yao ya kazi ikiwemo baadhi yao kukosa nyumba zilizopo ndani ya shule kwa usalama wao Zaidi,miundombinu ya kutembea kwa miguu kutokuwa rafiki kwao pamoja na kusahaulika katika kupata nafasi mbalimbali ambazo wanaamini wana uwezo wa kuwajibikia.


Akieleza changamoto zinazo wakabili ambazo zinahitaji kutatuliwa mapema ,Mwalimu Ally Sufiani kutoka shule ya Sekondari Moshi amesema kuwa zipo changamoto ikiwemo ukosefu wa nyumba za kuishi,njia za kuingia madarsani kutokuwa rafiki kwao pamoja na kusahaulika katika kupewa nafasi za uongozi ili hali wapo walimu wenye ulemavu wanaoweza kuongoza.


“Tuna fahamu kuwa serikali na Manispaa yetu ya Moshi imekuwa ikiendeleza jitihada za kutatua changamoto zetu sisi walimu wenye ulemavu ila tuna omba ziharakishwe katika kutatuliwa ili tuweze kufanya majukumu yetu vizuri pasipo usumbufu,tunahitaji kipaumbele katika kupata nyumba zilizo ndani ya shule kama walimu wengine,njia ya kuingia katika madarasa ziwe rafiki kwetu kwa kutembea au kutumia viti mwendo pamoja na kupewa nafasi za kuongoza maana wapo wenye uwezo” alishauri Sufiani.


Kwa upande wake Mwalimu Bi.Hawa Tuja kutoka shule ya Sekondari Moshi mwenye ulemavu wa viungo ameiomba serikali kuwakumbuka walimu wenye ulemavu ambao wanauwezo wa kushiriki michezo mbalimbali ili waweze kushiriki na kuleta hamasa kwa jamii kuona kuwa walemavu nao wanaweza kushiriki.

“Mimi ni Mwanamichezo,nimecheza timu ya Taifa mchezo wa Wheelchair tenes kwa sasa nimeajiriwa nipo Moshi na sija shiriki michezo tena, kwa kuwa ipo sera ya michezo ndani ya katiba ya  CWT naomba Walimu wenye ulemavu tupewe nafasi ya kushiriki michezo mbalimbali pamoja na ruhusa kutoka kwa viongozi wetu ili tuendeleze vipaji vyetu na kufundisha hata Watoto wenye ulemavu katika maeneo yetu” aliomba Bi.Tuja.


Awali akimkaribisha Mgeni rasmi katika kikao hicho Herry Christopher  Mwenyekiti wa CWT Manispaa ya Moshi amesema kuwa kikao hicho ni mahususi katika kufahamiana na kuelezana changamoto mbalimbali zinazo wakabili walimu wenye ulemavu ili ziweze kutatuliwa na kuwafanyia mazingira rafiki wakati wa kutumiza majukumu yao.

“Tunashukuru tumekuwa na Mkurugenzi anaye sikiliza na kutoa kipaumbe kwa walimu wenye ulemavu,wapo waliomba kusaidiwa kununua miguu ya bandia ili  kurahisisha  utendaji wao wa kazi na wamefanyiwa hivyo na ofisi ya Mkurugenzi,hata hizi changanoto nyingine zitatatuliwa kwa kushirikiana kati ya serikali na  Chama Cha Walimu (CWT) Manispaa ya Moshi” alisema


Kwa upande wake  mwalimu Bi.Hellen ambaye ni mwakilishi wa walimu wenye ulemavu ngazi ya Mkoa na Mjumbe wa baraza la Taifa wa Chama Cha walimu ameeleza kuwa nafasi zinazo ombwa na walimu wenye ulemavu ni zile zilizo ndani ya uwezo wao.


“Usimamizi wa mitihani ni ngumu kwa walimu wenye ulemavu kusimamia kulingana na zoezi hilo kuwa nyeti sana,mwalimu mwenye ulemavu wa kuona,kusikia au hata kutembea itamuwia vigumu kulifanya kwa ufanisi hata kama atakuwa na mtu wa kumsaidia bado panaweza kujitikeza shida lakini kwa nafasi nyingine tulizo na uwezo nazo tunaomba Serikali yetu ituhusishe” Bi.Hellen.


Akieleza kuhusu sera ya walimu wenye ulemavu iliyotungwa  na Chama Cha Walimu ya mwaka 2013, Katibu wa Chama Cha Walimu Mkoa wa Kilimanjaro, Daudi Mafwiri ameeleza kuwa  sera hiyo inaeleza kuhusu umuhimu wa kuwa na sera hiyo,malengo mahususi ya sera ya walimu wenye ulemavu na kuonesha tamko la sera kuhusu elimu kwa jamii kuhusu  huduma za walimu wenye ulemavu,takwimu za walimu wenye ulemavu, na kamati za walimu wenye ulemavu kwa ngazi zote kwa lengo la kuwatambua na kuwathamini kwa kuwapa mazingira mazuri katika kutekeleza kazi zao.


“Lengo kuu la Chama cha Walimu Tanzania ifikapo mwaka 2025 kuweza kutoa huduma bora kwa walimu wenye ulemavu na kuwawezesha kufanya kazi zao kwa ufanisi na ukamilifu katika shughuli za chama,kutambua mahitaji yao,nafasi za kutoa maamuzi na kuwa wawakilishi” alisema Mafwiri.


Aliongeza kuwa Changamoto zilizo wasilishwa na walimu hao wenye ulemavu zitaendelea kutatuliwa kupitia Chama Cha Walimu kwa kushirikiana na Serikali ili kufikia matamanio ya Chama hicho  na walimu wenye ulemavu kwa kuwa na mazingira bora na wezeshi.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Post a Comment (0)

 

 

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top