Ajali za barabarani zimetajwa kuwa ni chanzo kuu kinachopelekea watu wengi kupata ulemavu wa kudumu visiwani Zanzibar.
Akiwasilisha hotuba katika kilele cha maadhimisho ya kitaifa ya watu wenye ulemavu huko Uwanja wa Gombani ya kale Pemba, Makamo wa kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Massoud Othman, amesema matukio ya ajali za mara kwa mara za barabarani ni miongoni mwa sababu kuu zinazopelekea kuongozeka idadi ya watu wenye ulemavu, hivyo basi amewataka madera wa vyombo vya moto hususan bodaboda kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuepukana na ajali hizo.
"Takwimu zinaonesha watu wengi wamepata ulemavu kutokana na ajali za barabarani, unamkuta dereva anaendesha chombo huku akiwa anachati na kusababisha ajali za kizembe, hivyo basi niwaombe madereva wa vyombo vya moto hususan bodaboda kuzingatia sheria za usalama barabarani"
Aidha Mheshimiwa Othman, amesema suala la kuwapatia huduma bora watu wenye ulemavu ni takwa la kikatiba linalopaswa kuzingatiwa vyema katika utekelezaji wake, amesema kutokana na sheria hiyo Serikali ya jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar zimekuwa zikichukua hatua jitihada mbali mbali kuondosha matatizo yanayowakabili watu wenye ulemavu ikiwemo kubadili sheria na ujenzi wa majengo yanayozingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu.
Akizitaja miongoni mwa changamoto zinazowakabili watu wenye ulemavu ni pamoja na upungufu wa waalimu, vifaa katika elimu mjumuisho, miundombinu isiyo rafiki, uhaba wa wataalamu wa lugha ya alama, uwezeshaji kiuchumi pamoja na udhalilishaji hasa kwa watu wenye ulemavu wa akili.
Sambamba na hayo, amewaomba wananchi kubadili mfumo wa maisha hasa katika ulaji wa vyakula mbali mbali kwakuachana na vyakula vya mafuta, Sukari na uanga mwingi ili kupunguza uwezekano ili kuepukana na kupata maradhi yakuambukiza ambayo pia husababisha ulemavu.

Nae, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa kwanza wa Rais, Harusi Said Suleiman, ameitaka Jamii kuacha kuwaficha watoto wenye ulemavu kwani kufanya hivyo kuwanyima haki zao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa baraza la watu wenye ulemavu Zanzibar Bi. Salma Saadati, amesema watu wenye ulemavu wanapaswa kufunzwa na kuibua vipaji vyao vya aina mbali mbali ili waweze kuendelezwa na kutumika katika shughuli za kimaendeleo.
Mwakilishi wa Shirika la NFPA Bi. Amina, amesema Dunia ina watu bilioni moja kati ya watu bilioni nane, hivyo basi kuna haja ya kuwepo na mikakati na sheria imara ya kuwajengea mazingira bora watu wenye ulemavu Ili kuchangia katika kujenga uchumi wa Dunia.
Maadhimisho ya kitaifa ya watu wenye ulemavu duniani yamedhimishwa leo December 03 huko katika Uwanja wa Gombani ya kale, ambapo kauli mbiu ya mwaka huu inasema "SULUHISHO LA MAGEUZI KWA MAENDELEO JUMUISHI, JUKUMU LA UVUMBUZI KATIKA KUCHOCHEA ULIMWENGU UNAOFIKIWA KWA UWIANO"