Mahakama ya Wilaya ya Mufindi imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela pamoja na kazi ngumu Ayubu Nyigo mwenye umri wa miaka 30 kwa kosa la kumbaka mwanaye wa kumzaa mwanafunzi wa darasa la saba mwenye umri wa miaka 13
Ayubu Nyigo mkazi wa Kijiji cha Itimbo Kata ya Ifwagi Wilayani Mufindi alitekeleza tukio hilo tarehe 9/7/2022 majira ya saa nne za usiku alipotoka kirabuni kunywa pombe ambapo baada ya kufika nyumbani kwake alimfuata mwanaye chumbani alikokuwa amelala na wadogo zake kisha kwenda naye chumba kingine
Mhanga wa tukio hilo la ubakaji ambaye jina lake limehifadhiwa kwa sababu za kiusalama aliiambia mahakama kuwa baada ya kupelekwa chumba kingine baba yake alimvua nguo kisha nay eye kufungua zipu ya suruali na kumziba mdomo na hatimaye akaanza kutekeleza tukio hilo.
Mtoto huyo alieleza kuwa baada ya kufanyiwa kitendo hicho baba yake alitishia kumuua kama endapo angetoa taarifa mahala popote.
Lakini asubuhi ilipofika baada ya kuona anapata maumivu ya tumbo alienda kumweleza jirani yake ambaye ni mama yake mdogo kwani nyumbani hapo wanaishi yeye,wadogo zake na ba ba yake mama yake alitangulia mbele ya haki.
Baada ya kumweleza mama yake mdogo alilipeleka jambo hilo katika serikali ya kijiji na mtuhumiwa alikamatwa kisha kufikishwa mahakamani.
Baada ya kufikishwa mahakamani mtuhumiwa alikana kutenda kosa hilo licha ya kwamba uchunguzi wa daktari ulibaini kuwa mtoto huyo aliingiliwa kinguvu kwani alionekana anamichubuko katika sehemu zake za siri
Kesi hiyo ya jinai imesimamiwa na wakili wa serikali mwandamizi Twide Mangula na ilikuwa na mashahidi watatu.
Akisoma hukumu hiyo Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo Edward Uphoro amesema kutokana na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo mahakama imemtia hatiani Ayubu Nyigo na mtuhumiwa anastahili kifungo hicho ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye nia ovu kama hiyo
Hata hivyo mtuhumiwa alipopewa nafasi ya kujitetea aliiomba mahakama impunguzie adhabu lakini kutokana na ombi la upande wa mashtaka kuiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali,Mahakama imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela pamoja na adhabu ya kazi ngumu