Kituo cha Sheria na Haki za binadamu, wameiomba serikali kutunga sheria mahususi ya kupinga ukatili wa kijinsia au ukatili wa majumbani kwaajili ya kuhakikisha usalama zaidi wa wanawake dhidi ya ukatili wa kijinsia na ukatili wa majumbani.
Hayo ameyasema Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga wakati akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam katika kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia ambazo huadhimishwa kuanzia Novemba 25 hadi Disemba 10 .
Henga amesema kwa mwaka 2021 Tanzania imeshuhudia ongezeko la vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto wakiwa wahanga hivyo ameiomba serikali kuboresha huduma za jamii, haki na kuhakikisha wanawake wanapata msaada pale wanapofanyiwa ukatili.
"serikali iendelee kutoa elimu kwa jamii kuhusu hali za wanawake, watoto, wasichana na haki za binadamu kwa ujumla ili kuleta mabadiliko ya tabia lakini pia wanawake hao waweze kuwa na nyumba salama na huduma za kisaikolojia"
Henga ameliomba jeshi la polisi kuendelea kuboresha mifumo ya ukusanyaji taarifa kuhusu mauaji ya makusudi ya wanawake na kutengeneza miongozo inayozingatia hali halisi hasa katika ukusanyaji wa matukio ya mauaji ya wanawake kwa kuyatenganisha na mauaji ya kawaida.
Henga ameitaka jamii kupaza sauti zao kutokaa kimya dhidi ya aina yoyote ya ubaguzi na ukatili lakini pia kuachana na mila potofu na zilizopitwa na wakati zinazowaweka wanawake, wasichana na watoto katika hatari ya kufanyiwa ukatili.
Mbali na hayo, Henga amesema endapo mifumo kandamizi na mila potofu ikiwemo fikra potofu zinazowanyima wanawake uhuru wa kutoa taarifa za ukatili ilibadilishwa, itasaidia kuwajengea uwezo watoa huduma ili watoe huduma rafiki kwa wahanga.
"Wanawake toeni taarifa kuhusu ukatili hata pale mnapoona wenzenu wanafanyiwa na kutoa misaada kwa wenzenu kwa kuacha kusimamia mfumo dume na kandamizi"