Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la Richard Nzumbe (32) mkazi wa mtaa wa Butengwa Manispaa na Mkoa wa Shinyanga ameuawa kwa kupigwa risasi sehemu mbalimbali za mwili wake na watu wanaosadikika kuwa ni majambazi.
Tukio hilo limetokea Desemba 19,2022 majira ya saa 1 usiku katika Kata ya Ndembezi, Mtaa wa Butengwa, Manispaa ya Shinyanga.
Akieleza juu ya tukio hilo Mwenyekiti wa Mtaa Butengwa, Onesmo Mayeba, Amesema majira ya saa 1 usiku alipewa taarifa na majirani juu ya tukio hilo ambapo alifika eneo husika na kukuta majambazi hao wamekwisha tenda uvamizi huo huku ikisemekana lengo la kufanya uvamizi huo ni kuwania fedha kutoka kwa mfanyabiashara huyo.
Awali akieleza undani wa tukio hilo Shemeji wa marehemu,Salome Dady, amesema majira ya saa 1 usiku walikuwa ndani yeye na watoto wa dada yake,ndipo waliposikia gari la shemeji yake likiwa limefika getini ambapo mtoto wake alienda kufungua geti ndipo aliposukumwa na majambazi hao na kumfuata marehemu kisha kumfanyia unyama huo.
"Tulikuwa ndani mimi na watoto wa dada mara tukasikia gari likiwa getini ambapo alienda mtoto wa dada kufungua mlango ndipo nikasikia kelele nje ikabidi nitoke nikaone kuna nini nikakuta watu wawili wanampiga risasi shemeji nikachukuwa kigoda nikampiga kichwani mmoja wa majambazi hao akaanguka kisha nikafata kisu jikoni na kumchoma mwingine, ndipo walipoamua kukimbia"Amesema Salome Dady.
Kufatia tukio hilo Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa Shinyanga,ACP,Janeth Magomi Amethibitisha kutokea kwa tukio hilo ambapo amesema Jeshi la polisi linaendelea na msako wa kina kuwabaini waliohusika na tukio hilo na kuwahasa wafanyabiashara kuacha mazoea ya kukaa na fedha nyumbani bali wahifadhi kwenye mabenki.
BOFYA HII VIDEO HII KUTAZAMA KWA UNDANI